MASIGNCLEAN101

MAENDELEO YA KISWAHILI

MAENDELEO YA KISWAHILI
citylab
Thursday 20 February 2020

Kiswahili ni lugha inayozungumzwa katika eneo kubwa la Afrika ya Mashariki. Lugha hii ina utajiri mkubwa wa misamiati, misemo, mithali, mashairi, mafumbo, vitendawili na nyimbo. Kiswahili hutumika mashuleni, katika mawasiliana na kuna vitabu vingi vilivyotungwa kwa kutumia lugha hiyo, vikiwa pamoja na vile vya hadithi, hekaya au riwaya.
Lugha ilianza takriban miaka 800-1000 iliyopita katika pwani ya Afrika Mashariki.Wakazi wa Pwani hii waliokuwa wasemaji wa lugha za Kibantu tofauti tofauti mfano; kisukuma, kihaya, kijita, kikurya, kimakonde, kingoni, kihehe, kizigua, kibena n.k.katika shughuli mbalimbali kama biashara ambazo zilikuwa zikiwakutanisha watu hawa wakiwa wanaozungumza lugha tofauti tofauti, iliwabidi waweze kuchukua msamiati mbalimbali kutoka katika lugha zao ili waweze kuwasiliana katika shughuli zao. Walipopokea maneno mengi hasa ya Kibantu katika mawasiliano yao, ikachangia kuwa msingi wa Kiswahili ni sarufi na msamiati wa Kibantu.
Kwakua tumeona kuwa Kiswahili ni lugha sasa basi, lugha nini?
Lugha ni sauti za nasibu zilizo katika mpangilio maalumu na zilizo kubaliwa na jamii ya watu zitumike kama chombo cha mawasiliano.
Au
Ni mfumo wa sauti za nasibu za kusemwa zinazotumiwa na watu wa jamii fulani wenye utamaduni unaofanana kwa madhumuni ya mawasiliano katika jamii hiyo.
Au
Katika kamusi ya kiswahili sanifu TUKI 1981 oxford press uk. 86, inafafanua kuwa lugha ni mfumo wa sauti nasibu ambazo hutumiwa na jamii kwa madhumini ya mawasiliano kati yao.
Sifa / tabia za lugha.

  • (a)Lugha huzaliwa.
  • Lugha huzaliwa kutokana na mwingiliana kati ya lugha mbili au zaidi nakutengeneza lugha moja. Kwa mfano lugha ya Kiswahili imetokana na mwingiliano wa lugha mbalimbali za kibantu.
  • (b)Lugha hukua.
  • Lugha hukuwa kutokana na kuongezeka kwa msamiati mbalimbali ambayo hutumiwa katika lugha husika katika shughuli mbalimbali.
  • (c)Lugha huathiliwa.
  • Lugha huathiliwa kutokana na mwingiliano wa lugha mbili tofauti  na kusababisha ukiukwaji wa kanuni na matumizi sahihi ya lugha mojawapo. Kwamfano Kiswahili kinaweza kuathiliwa na kiingeleza pale ambapo mtumiaji au watumiaji wanapochangaya maneno ya kiingereza katika Kiswahili, pia kutumia sarufi ya lugha ya kiingereza pindi atumiapo lugha ya Kiswahili.
  • (d)Lugha hufa.
  • Lugha hufa kutokana na kukosekana kwa msamiati wa lugha husika.
  • (e)Lugha ina ubora.
  • Ubora wa lugha hupatikana kwa watumiaji wa lugha yenyewe. Kwa mfano,kiwahili kinaubora kwa Wakazi wa Afrika Mashariki kwasababu ndio watumiaji wa lugha hiyo.
  • (f)Lugha ni sauti za kusemwa na binadamu.
  • Mwanadamu hutumia alama za sauti kimsingi hakuna kiumbe ambacho si binadamu kinachoweza kuzunghumza lugha.
  • CHIMBUKO LA LUGHA YA KISWAHILI.
  • Chimbuko ni asili ya kitufulani, tunaposema chumbuko la lugha ya kiswahili tunaangalia asili ya lugha ya kiswahili. Yawezekana kabisa kuwa kila jamii inahistoria yake jinsi lugha yake ilivyozuka, vivyo hivyo hata kiswahili kina asili yake kamaifuatavyo:
  • KISWAHILI NI KIKONGO, katika hoja hii tunaona kuwa hapo zamani Pwani ya Afrika Mashariki ilikuwa ombwe (hapakuwa na kitu) wakongo walifika wakiwa katika misafara yao na kuweka kambi kisha makazi. Baada ya wakongo hawa kuwa na makazi imegundulika kuwa lugha iliyokuwa ikizungumzwa ilihusiana na lugha ya Kiswahili. Katika hoja hii tunapata ukakasi unaosababisha tushindwe kupata uthibitisho wakisayansi unaoonesha kuwa kiswahili nikikongo.
  • KISWAHILI NI LUGHA YA VIZALIA, Vizalia ni watoto ambao walitokana baada ya mwingiliano wa wanawake wa Afrika mashariki na waarabu waliokuwa wakifika Pwani ya Afrika Mashariki kwa madhumuni ya kufanya biashara. Baada ya mwingiliano huo walioaona na kuzaa watoto ambao walichukuwa baadhi ya maneno (misamiati) kutoka kwa Baba zao na kwa Mama zao kisha kutumia katika mawasiliano na kuwa lugha moja iliyojulikana kama lugha ya vizalia.
  • KISWAHILI NI PIJINI,  wakazi wa afrika Mashariki waliingiliana na Waarabu waliofika kwa ajili ya biashara zao wakakuta lugha inayozungumzwa ni tofauti na lugha yao ndipo ilipozuka lugha ya Kiswahili kwa kuchukua maneno kutoka katika lugha zote mbili na kuunda lugha moja ambayo ni pijini ambayo waliitumia katika mawasiliani yao. Kwakua lugha hii ilikuwa ikitumiwa na wakazi hawa ilionekana kuwa ndilo chimbuko la kaswahili, lakini hoja hii inakosa mashiko kwani inatupatia uthibitisho wa nadharia pekee hatujapata uthibitisho wa kisayansi unaoonesha kuwa pijini ndilo chimbuko la kiswahili.
  • KISWAHILI NI KRIOLI,  hii ni pijini iliyokomaa. Baada ya pijini kuendelea kutumika na watumiaji wake na kuwa lugha Mama ya jamii husika huitwa krioli.
  • KISWAHILI NIKIARABU, kuna thibitisho mbalimbali ambazo zinathibitisha kuwa Kiswahili kimetokana na lugha ya kiarabu, uthibitisho huo ni:
  • Kutokana na neno lenyewe KISWAHILI neno hili limetokana na neno la kiarabu “sahili”umoja na wingi wake ni “Swahili”lenye maana ya Pwani ya Afrika mashariki. Kwakua neno hili ni lakiarabu na warabu walifika Pwani ya Afrika Mashaiki kwaajili ya biashara zao ikathibitiashwa kuwa kiswahili asili yake ni kiarabu.
  • Kiswahili kilitumika katika dini ya kiislam, baada ya Waarabu kufika uwanda wa Pwani ya Afrika mashariki kuendesha biashara zao pia walikuja kueneza dini ambayo ni kiislamu. Dini hiyo ilienezwa kwa lugha ya kiswahili kwa wakazi wa Pwani. Kufuatia kuenea kwa dini hiyo ikachangia kueneza lugha ya kiswahili na kuthihirika kuwa kiswahili chimbuko lake ni kiarabu.
  • Baadhi ya maneno yaliyomo na yanayotumika katika lugha ya Kiswahili ni ya kiarabu. Kwamfano maneno kama siri, gati, sukari nk, maneno haya yanatumika katika lugha ya kiswahili na nimisamiati sanifu. Inakadiliwa kuwa lugha ya kiarabu inamaneno asilimia 31 katika lugha ya Kiswahili ambayo hutumika katika muktadha mbalimbali. Kutokana na uthibitisho huo inadhihilishwa Kiswahili ni kiarabu.
  • KISWAHILI NIKIBANTU
  • Neno KIBANTU limetokana na neno BANTU maana yake ni WATU. Wabantu hupatikana Afrika haswa Afrika mashariki na kati ikihusisha mataifa kama Tanzania, Rwanda, Burundi, Kongo, Kenya  n.k
  • Tunaposema kiswahili ni kibantu ina maana kuwa, lugha ya kiswahili ni lugha ambayo imetokana na muunganiko wa misamiati ya lugha za makabila mbalimbali yanayopatikana afika mashariki na kati, kwamfano Kisukuma, kihaya, kijita, kingoni kihehe na n.k.
  • Dhana hii imeonekana kuwa na mashiko na kuweza kutoa udhibitisho wakisayansi unaothihilisha asili ya kiswahili nikibantu, yaani kimetokana na muunganiko wa misamiati kutoka katika lugha mbalimbali. Ili kuthibitisha hoja hii kunauthibitishoi wa KIISIMU na ule wa KIHISTORIA
  • USHAHIDI WA KIISIMU.
  • Isimu ni sayansi ya lugha. Tunaposema sayansi ya lugha ni jinsi ambavyo lugha ilivyopangiliwa ki muundo, kimatamshi, kimaana na kimtindo.
  • Tutaendelea kutazama kwanini tunasea kiswahili ni kibantu usikose……………………….!!
  • Kukua na kuenea kwa kiswahili wakati wa ukoloni 
  • Form 3 Kiswahili 

  • Wakoloni na ukoloni Afrika Mashariki
  • Katika karne ya kumi na tisa Afrika Mashariki iliingia kwenye mahusiano na mataifa mengine kama vile Marekani, Ujerumani na Uingereza. Mahusiano haya ni baada ya watu wa pwani kuwa na uhusiano wa muda mrefu wa kibiashara na Waaarabu, hawa waliweka athari kubwa katika kukua na kuenea kwa lugha ya Kiswahili. Wageni kutoka Ulaya walipoingia Afrika Mashariki walifanya biashara, shughuli za kidini (mishenari), elimu na utawala. Kama ilivyokuwa katika kipindi cha Waarabu, uwepo wao pia ulikuwa na athari katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili Afrika Mashariki na kwingineko.
  • Maendeleo ya Kiswahili kipindi cha waarabu
  • Waarabu hasa katika pwani ya Afrika Mashariki walifanya biashara ikiwemo biashara ya watumwa. Ilikuwepo misafara mbalimbali ya biashara kutoka pwani hadi bara. Katika misafara hiyo Kiswahili ndio ilikuwa lugha ya mawasiliano hivyo Kiswahili kikaenea pia katika sehemu za bara.
  • Kuna mambo kadhaa waliyofanya waarabu ambayo yalichangia kukua kwa lugha ya Kiswahili. Waarabu walichangia kukua kwa lugha ya Kiswahili kama ifuatavyo:
  • Biashara  
  • Waarabu walifanya biashara kati ya pwani na sehemu za bara, katika biashara yao walichangia kwa kiasi kikubwa uenezaji wa lugha ya Kiswahili. Lugha kuu ya mawasiliano na ya kibiashara iliyotumiwa na wafanya biashara wa kiarabu ilikuwa ni Kiswahili, kwa hiyo kwa njia hii waliweza kueneza Kiswahili kuanzia pwani hadi maeneo ya bara kama vile Tabora, Kigoma hadi mashariki mwa Kongo.
  • Dini
  • Dini pia ni jambo ambalo liliweza kuchangia ueneaji wa lugha ya Kiswahili enzi za waarabu. Waarabu walipokuja walitaka kueneza dini yao kwa undani kabisa. Kwa hivyo iliwabidi kuanzisha madarasa ambayo walitumia kufundishia, lugha iliyokuwa ikitumiwa ni lugha ya Kiswahili. Na hivyo hii ikasaidia kuenea kwa lugha ya Kiswahili.
  • Maandishi ya kiarabu
  • Waarabu pia walileta hati zao zilizotumiwa katika maandishi ya lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo kupitia hati za kiarabu maandishi mbalimbali ya lugha ya Kiswahili yaliweza kuhifadhiwa, hivyo Kiswahili kiliweza kukua kwa vile kingeweza kuhifadhiwa katika maandishi na kusomwa wakati wowote.
  • Kuoana
  • Pia vilevile Waarabu waliofika pwani waliweza kuoana na wabantu, hii ilisababisha kizazi kipya kutokea.  Na  kwa sababu hiyo watoto walichukua maneno mengi kutoka kwa baba na mama yao na hivyo kuongeza msamiati katika lugha  Kiswahili.
  • Maendeleo ya Kiswahili kipindi cha wajerumani
  • Wajerumani waliingia katika pwani ya Afrika Mashariki katika miaka ya 1875, walifanya kila jitihada kuwatawala Waafrika ambapo katika utawala wao walifanya biashara, waliendesha shughuli za kiutawala, za kidini na kielimu. Katika shuguli zote hizo Kiswahili ndio ilikuwa lugha ya mawasilino hivyo kukikuza na kukiendeleza Kiswahili.
  • Walipongia katika pwani ya Afrika Mashariki walikuta Kiswahili kimekwisha enea kwa kiasi kikubwa. Kuna mambo waliyoyafanya ambayo yalisaidia kukua na kuenea kwa Kiswahili kama ifuatavyo:
  • Kutoa mafunzo ya lazima ya lugha ya Kiswahili kwa wafanya kazi wa serikali
  • Waliwalazimisha wafaanyikazi wote wa serikali kujifunza kiswashili, kwa sababu sheria ilikuwa ni kwamba pasipojua Kiswahili huwezijiriwa katika serekali ya mjerumani. Kwa hiyo saula hili lilisababisha watu kujifunza lugha ya Kiswahili ili waweze kuajiriwa. Wafanyakazi ambao ilikuwa ni lazima wajifuze Kiswahili ni pamona na maakida.
  • Wajerumani wenyewe walilazimika kujifunza kiswahili  ili waweze kuwasiliana na wenyeji kwa urahisi na hivyo kurahisisha shuguli zao za kiutawala.
  • Ujenzi wa shule
  • Shule zilifunguliwa kufundisha watu weusi ili waje wawe wasidizi wao katika utawala wa wajerumani, na lugha iliyokuwa ikitumika kufundisha masomo ilikuwa ni lugha ya Kiswahili.
  • Kuenea kwa utawala wa Wajerumani nchi nzima
  • Utawala wa wajerumani ulikuwa kwenye kila kona ya nchi. Na kwa kuwa wafanya kazi wa serikali ya wakati huo ilikuwa ni lazima wafahamu Kiswahili, kwa hiyo kila sehemu palipokuwa na ofisi za serikali nchi nzima kulizungumzwa Kiswahili.
  • Shughuli za kiuchumi
  • Pia katika shuguli za mashamba, wajerumani walichukua vibarua kutoka sehemu mbalimbali za nchi, na kwa kuwa kila mmoja alikuwa na lugha yake tofauti, kwa hiyo lugha pekee iliyowaunganisha katika mawasiliano kwenye eneo la kazi ilikuwa ni Kiswahili.
  • Kwa hiyo kutokana na sababu kwamba utawala wa kijerumani ulitoa msukumo mkubwa katika matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye shughuli zao za kiutawala, hivyo suala la ueneaji wa Kiswahili lisingeepukika.
  •  http://www.shuledirect.co.tz/notes/view_notes/74
  • Ukuaji na ueneaji wa Kiswahili katika enzi za Waingereza 
  • Form 4 Kiswahili 
  • Mambo yaliyosaidia ukuaji wa Kiswahili enzi za utawala wa Waingereza
  • Waingereza walipochukua koloni la Tanganyika kutoka kwa Wajerumani walikuta Kiswahili kimeimarika na kinatumika katika maeneo mengi ya nchi. Kwa kuwa nao walihitaji kutawala hawakupuuzia matumizi ya Kiswahili katika utawala wao japo hawakutumia Kiswahili kwa lengo la kukikuza lakini walijikuta wanakieneza na kukikuza bila ya wao kukusudia.
  • Waingereza walitumia Kiswahili kama nyenzo ya kusaidia shughuli zao za kiutawala. Hata hivyo kuna mambo waliyofanya waingereza yaliyosaidia kukua na kuenea kwa Kiswahili, mambo hayo ni kama yafuatayo:
  • Shuguli za kiuchumi 
  • Shuguli za kiuchumi wakati wa Waingereza zilihusisha kilimo na biashara. Kwa upande wa klimo, Waingereza waliendesha kilimo cha mazao mbalimbali, na walitumia mfumo wa kuajiri vibarua kutoka sehemu mbalimbali za nchi. Vibarua hao walijulikana kwa jina la manamba.
  • Katika mkusanyiko wa vibarua hawa waliokuwa na usuli wa makabila tofautitofauti, lugha pekee iliyoweza kuwaunganisha ni Kiswahili ikizingatiwa kwamba Kiswahili kiliteuliwa kuwa lugha rasimi katika mawasiliano ya kiutawala. Walilazimika kuzungumza Kiswahili kwani bila hivyo mawasiliano yasingeweza kufanyika kwa urahisi.
  • Hata hivyo kupitia shuguli za kilimo maneno mapya ya Kiswahili yaliweza kuzaliwa, kwa mfano: yadi, belo, belingi, bani, mtama n.k, kwa hiyo kupitia shughuli hizi Kiswahili kilizidi kukua.
  • Shuguli za kiutamaduni 
  • Shughuli hizi ni kama vile uigizaji wa tamthiliya za kigeni, uchezaji wa mziki wa kigeni hususani twisti. Tamthiliya za kigeni zilikuwa zikiigizwa majukwaani kwa lugha ya Kiswahili na hivyo ikasaidia kukua kwa msamiati wa Kiswahili.
  • Shughuli za kidini 
  • Wakati wa utawala wa mwingereza pia kuliambatana na ujio wa wamishonari waliokuwa na lengo la kueneza dini ya kikristo.
  • Katika harakati hizi walitumia lugha ya Kiswahili ili kufanikisha malengo yao ikizingatiwa kwamba Kiswahili kilikuwa kimeshaenea vya kutosha wakati wa utawala wa Mjerumani, kwa hiyo wamishonari wa Kiingereza waliendelea kukiimarisha zaidi.
  • Pia shughuli za kidini zilipelekea kutafsiriwa kwa vitabu mbalimbali vya kidini kama vile Biblia na vitabu vingine. Tafsiri ya vitabu hivi ilikuwa ni kutoka katika lugha ya kiingereza kwenda katika lugha ya Kiswahili. kwa kufanya hivi Kiswahili kiliweza kuingiza msamiati mwingi sana na hivyo kukuza lugha ya Kiswahili.
  • Wamishonari walilazimika kujifunza Kiswahili hukohuko kwao ili wanapokuja huku Afrika Mashariki wasipate tabu ya kujifunza Kiswahili. Kwa sababu hii wamishonari waliokuwa wamekwishajifunza lugha ya Kiswahili walitunga kamusi za Kiswahili – Kiingereza   ili kuwasaidia wenzao pia kujifunza Kiswahili; kwa njia hii waliweza kukikuza Kiswahili.
  • Shughuli za kisiasa 
  • Shughuli za kisiasa hasa katika uanzishwaji wa vyombo mbalimbali vya kiutawala, jeshi, polisi, mahakama, boma n.k. Kufuatia uanzishwaji wa vyombo hivi msamiati mwingi wa Kiswahili uliweza kuzuka na hivyo kukuza Kiswahili.
  • Shughuli za kiutawala
  • Makampuni ya uchapishaji yalianzishwa (East African literature Bureau), na kamati ya lugha iliundwa (Interterritorian language committee). Hatua hii iliimarisha matumizi ya lugha ya Kiswahili hali iliyosaidia kukua kwa lugha ya Kiswahili.
  • Shuguli za ujenzi wa reli na barabara
  • Shughuli hizi pia zilisaidia kuibuka kwa msamiati mpya kama vile, reli, stesheni, tiketi n.k.
  • Usanifishaji wa Kiswahili 
  • Usanifishaji wa lugha ya Kiswahili pia lilikua ni jambo jingine muhimu sana lililosaidia kukua kwa msamiati wa Kiswahili. Lengo la usanifishaji wa Kiswahili lilikuwa ni kuleta ulinganifu wa matumizi ya lugha ya Kiswahili katika ukanda wa Afrika Mashariki. 
  • UENEAJI WA KISWAHILI 
  • Ukuaji na Ueneaji ni maneno mawili yenye maana zinazokaribiana lakini zinazotofautiana. Ukuaji humaanisha ongezeko la msamiati katika lugha na ueneaji ni uongezekaji wa matumizi ya lugha kieneo. Kwa hiyo hapa tutaangalia yale mambo yaliyosababisha Kiswahili kitumike katika eneo kubwa. Mambo hayo ni haya yafuatayo:
  • Vyombo vya habari
  • Vyombo vya habari vilivyokuwepo kwa wakati huo ni redio, magazeti na majarida mbalimbali. Kwa upande wa redio kulikuwepo na redio Tanganyika iliyoanza kurusha matangazo yake kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Na magazeti yaliyokuwa yakichapishwa wakati huo ni pamoja na: Mambo leo, Sauti ya Pwani, Kiongozi na Habari za leo. Magazeti haya yote yalikuwa yakichapishwa kwa lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo kwa kutumia vyombo vya habari (redio na magazeti) kiswahili kiliweza kuenea.
  • Kilimo
  • Kupitia kilimo watu waliweza kukutana pamoja, watu wa makabila tofautitofauti. Kwa hiyo katika kipindi chote walichokaa kwenye makambi ya mashambani waliweza kujifunza Kiswahili na walipomaliza muda wao walirudi nyumbani wakiwa wamejifunza lugha mpya na hivo kwa njia hii waliweza kuieneza lugha ya Kiswahili.
  • Muundo wa jeshi la kikoloni (KAR)
  • Jeshi la KAR liliundwa na watu kutoka makabila mablimbali, na lugha iliyokuwa ikitumika jeshini ni Kiswahili, askari hawa walisaidia kueneza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi kwani kila walipokwenda walikuwa wakizungumza Kiswahili.
  • Mfumo wa elimu
  • Chini ya utawala wa Waingereza Kiswahili kilitumika katika masomo yote kwa ngazi ya shule ya msingi, na pia kilitumika kama somo kwa ngazi ya shule za sekondari. Kwa hiyo hii pia ilichangia kuenea kwa lugha ya Kiswahili.
  • Harakati za kudai uhuru
  • Chama cha TANU kilianzisha harakati za kudai uhuru, harakati hizo ziliendeshwa kwa lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo kupitia harakati hizo Kiswahili kiliweza kuenea kwa kiwango kikubwa.
  • Tathimini ya maendeleo ya Kiswahili wakati wa Waingereza
  • Licha ya maendeleo ya lugha ya Kiswahili katika utawala wa Waingereza, pia kulikuwa na changamoto zilizoikabili lugha ya Kiswahili katika kupiga hatua ya maendeleo. Changamoto hizo ni kama zifuatazo:
  • Kutofundishwa kwa Kiswahili shule zote nchini
  • Wakati wa utawala wa Waingereza Kiswahili kilifundishwa katika shule za watoto wa kiafrika tu, wakati katika shule za watoto wa kizungu Kiswahili hakikufundishwa. Kwa hiyo suala hili lilifanya Kiswahili kipewe msukumo mdogo sana na hivyo kuhafifisha ukuaji wake.
  • Kutotumika kwa Kiswahili kama lugha ya kufundishia
  • Lugha ya Kiswahili ilitumika kufundishia katika shule za msingi pekee ilihali lugha ya kiingereza ilitumika kuanzia shule za sekondari hadi elimu ya juu. Hali hii ilisababisha watu kujitahidi sana kujifunza kiingereza; kwa kuzungumza kiingereza ilikuwa na ishara kwamba wewe ni msomi, na hivyo kutokana na hali hii Kiswahili kilendelea kukua polepole sana.
  • Kukosekana kwa vyombo vya kizalendo vya kukuza Kiswahili
  • Vyombo vilivyokuwa vinahusika na masuala ya ukuzaji wa Kiswahili wakati wa ukoloni vilikuwa vimeanzishwa na wakoloni wenyewe, kwa mfano Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki (Inter-Territorial Swahili Language commitee) na Shirika la maandiko la Afrika Mashariki (East African Literature Bureau). Katika hali kama hii ukuzaji wa Kiswahili ulikosa msukumo mkubwa wa kizalendo.
  • Kasumba ya kuthamini Kiingereza
  • Wananchi walikuwa na kasumba kwamba mtu anayezungumza Kiingereza alichukuliwa kuwa ni mtu mwenye maendeleo na msomi, kwa hiyo hali hii ikapelekea watu kutothamini Kiswahili na hivyo Kiswahili kudharaulika.
Share This :
...