Monday, 9 March 2020
Maendeleo ya Kiswahili
KISWAHILI: HISTORIA NA MAENDELEO
1. Kiswahili kabla ya Ukoloni
Historia ya lugha ya Kiswahili imeanza kabla ya miaka ya 1000 BK kwenye pwani ya Afrika Mashariki. Kuenea kwake kabla ya ukoloni kulisababishwa na shughuli zakibiashara miongoni mwa Waafrika. Biashara hii, ilikuwa imeshamiri sana katika upwa wote wa Afrika Mashariki. Wenyeji wa maeneo haya, walikuwa na mawasiliano ya muda mrefu kabla ya kufika kwa wageni wa Kiarabu na Kizungu. Kulikuwa na safari zakibiashara baina ya pwani na bara zilizokuwa zikifanywa na Waafrika wenyewe. Katika safari hizo, watu wa bara waliofika pwani walijifunza na walikitumia Kiswahili cha pwani na kukieneza waliporejea kwao. Hao ndio walioanza, bila kukusudia, kuieneza lugha ya Kiswahili kutoka pwani hadi sehemu za bara. Waswahili waliendeleza misafara ya kibiashara hadi nchini Kongo na maeneo mengine ya Afrika ya Kati.
2. Kiswahili katika kipindi cha Ukoloni
Wageni walioshirikiana na wenyeji katika kueneza Kiswahili Afrika Mashariki wakati wa ukoloni ni Waarabu, Waajemi, Wareno, Wajerumani na Waingereza. Sababu zilizowafanya wageni hawa waje Afrika Mashariki ni kufanya biashara, kueneza dini nakutawala. Katika karne ya 19 BK wakoloni walifika katika bandari za pwani wakatumia mara nyingi makarani, askari na watumishi kutoka eneo la pwani na kujenga vituo vyao bara. Watu hawa walisaidia kukipeleka Kiswahili katika pande za bara. Kiswahilikilikuwa lugha ya utawala katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Wakoloni walitumia kazi za Wamisionari wa awali hasa Ludwig Krapf aliyewahi kufanya utafiti wa lugha na kutunga kamusi na sarufi za kwanza pamoja na kuleta mfumo wa kuandikaKiswahili kwa herufi za Kilatini.
Kukua kwa lugha ya Kiswahili kulikosababishwa na shughuli za kiutawala na kibiashara kulisababisha kuingia kwa maneno mengi mapya katika Kiswahili.Kiswahili kimeonyesha uwezo mkubwa wa kupokea maneno kutoka lugha tofauti kikitumia maneno haya kufuatana na sarufi ya lugha za Kibantu. Kwa jumla Kiswahili kina maneno mengi yenye asili ya Kiarabu ambayo inakadiriwa kuwa kati ya 30% na 40%. Hali hii ni kutokana na uhusiano ya muda mrefu baina ya pande hizi mbili na pia kutokana na lugha hii kuwekwa kwenye maandishi kwa kutumia herufi za Kiarabu tangu karne ya 13 BK. Hata hivyo, Kiswahili ni lugha yenye asili ya Kibantu kwa kutumia hoja za kiisimu na kihistoria.
Wafanyakazi kutoka makabila mbalimbali katika ujenzi wa reli, ufanyaji kazi katika mashamba makubwa yaliyozalisha mazao ya biashara, na katika migodi watu wa makabila mengi walitumia Kiswahili. Kwa namna hiyo lugha ya Kiswahili ilienea zaidi. Ili kuendesha shughuli zake, serikali ya kikoloni ya Waingereza iliona haja ya kuwa na lugha moja ambayo ingetumika katika makoloni yao yote ya Afrika Mashariki. Hata hivyo lugha ya Kiswahili ilikuwa na lahaja nyingi sana zilizoenea katika mwambao wote wa Afrika Mashariki na baadhi ya sehemu za bara. Kulikuwa na haja ya kuwa na lahaja moja ambayo ndiyo ingefanywa lugha rasmi.
Ili kukidhi haja hiyo, kamati maalumu ya kushughulikia suala hilo iliyojulikana kama kamati ya lugha ya Afrika Mashariki iliundwa. Mwaka 1929 Katibu wa halimashauri ya magavana wa Afrika Mashariki aliziandikia serikali nne kuhusu suala la kuanzishwa kwa kamati ya lugha ya serikali zote nne na tarehe 1-1-1930 kukaanzishwa kamati iliyoitwaInter-Territorial Language (Swahili) Committee ili ihusike na kusanifisha Kiswahili. Kamati hii iliiteua lahaja ya Kiunguja kuwa msingi wa lugha rasmi yamaandishi. Suala hili lifuatiwa na uchapishaji wa kamusi na vitabu vya sarufi.
3. Nafasi ya Kiswahili Duniani
Kiswahili sanifu siyo tena lahaja ya Kiunguja kama ilivyochukuliwa kitambo, bali ni lugha rasmi ya Kiswahili inayotumiwa na watu wengi sana Afrika Mashariki na Kati. Kiswahili sanifu kina msamiati na istilahi za taaluma mbalimbali. Kimeandikiwa kwamapana na kinatumika na watu mbalimbali katika sehemu nyingi za dunia. Lugha hii ina uwezo mkubwa sana wa kukabiliana na mazingira mapana zaidi na mabadiliko ya kisayansi na kiteknolojia. Nchi za Afrika ya Mashariki, hasa Kenya, Uganda na Tanzania ni nchi ambazo zimekuwa na uhusiano wa karibu tangu zamani. Zimekuwa na ushirikiano kihistoria na zote zilitawaliwa na Uingereza, hali iliyosaidia kuanzishwakwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki wakati wa uhuru. Lugha hii imekuwa ya watu wengi mijini na vijijini hasa Tanzania na Kenya. Kiswahili kinatumika pia Kaskazini mwa Msumbiji, Somalia, Kongo, Rwanda, Burundi, Sudani, na maeneo ya Malawi na Zambia.
Leo, lugha hii ina umuhimu mkubwa kwa sababu ya kuenea na kukusanya watu wa makabila na nchi kadha wa kadha wakaweza kufahamiana kwa lugha moja. Pia imekuwa ikitumiwa katika kusambaza habari katika vituo na mashirika mbalimbali vyahabari duniani. Kuna taasisi zinazolenga kukuza na kuimarisha Kiswahili kama vile Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) nchini Tanzania, Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA), nchini Kenya kuna Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA). Pia kuna Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na idara za Kiswahili katika vyuo vikuu mbalimbali vya Tanzania, Kenya naUganda na vyuo vikuu vingi duniani.
3.1. Afrika Mashariki
Baraza la Kiswahili la Taifa BAKITA (Tanzania), Chama cha Kiswahili cha Taifa CHAKITA (Kenya) na wawakilishi kutoka Uganda walianzisha wazo la kuundwa kwa Baraza la Kiswahili la Afrika Mashariki. Wazo hili liliongoza katika kuanzisha Kamisheni ya Lugha ya Kiswahili ambayo ilianza mwaka 2012. Hii ni kwa sababu Kiswahili ndiyo lugha ya Afrika Mashariki yenye uwezo wa kuwaunganisha watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inasimamia ukuzaji na maendeleo ya matumizi ya Kiswahili kwa ajili ya umoja wakikanda pamoja na maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa nchi zote. Lengo lake ni kukuza Kiswahili kiwe lugha ya matumizi mapana katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ushirikiano wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umeiwezesha lugha hii kukua na kusambaa sehemu kubwa ya ukanda huu. Pamoja na hayo, hadhiya Kiswahili inapanda na kukua kwani kinatumika katika mikutano mingi zaidi ya Kimataifa kama ilivyo sasa katika Umoja wa Afrika.
3.1.1 Tanzania: Nchini Tanzania, Kiswahili ni lugha ya taifa; lugha rasmi katika shughuli za serikali na bunge, lugha inayotumika kufundishia Shule za Msingi nakama somo katika elimu ya juu. Hata hivyo, sera ya elimu ya 2015 (tamko la 3.2.19) imeidhinisha rasmi matumizi ya Kiswahili katika mfumo wote wa elimu kuanzia Shule za Msingi hadi Vyuo Vikuu. Kiswahili kinatumika kutoa mafundisho ya dini makanisani na misikitini. Kiswahili ni lugha kuu inayotumika katika vyombo vya habari kama vile televisheni, redio na katika idadi kubwa ya magazeti ikiwemo mitandao mbalimbali ya kijamii.
3.1.1.1 Kiswahili na harakati za ukombozi Tanzania
Kiswahili kilitumika kama lugha ya mawasiliano katika harakati za siasa za kudai uhuru; mathalani mikutano ya vyama vya siasa kama vile ya Tanganyika African Association (TAA) iliendeshwa kwa lugha ya Kiswahili. Aidha, matumizi ya lugha ya Kiswahilikatika harakati hizi yalipanuka zaidi wakati wa kuundwa kwa chama cha siasa cha TANU 1954, ambacho viongozi wake akiwemo Mwalimu Julius Nyerere walihutubia wanachama wa chama hicho kwa Kiswahili. Safari za viongozi za kuzunguka Tanganyika nzima ili kuhamasisha Watanganyika kuunga mkono harakati za kudai uhuru zilifanywa kwa lugha ya Kiswahili. Jambo hili lililofanya Kiswahili kienee nakipate mashiko nchini Tanganyika. Pia, nyimbo za siasa zilizotungwa kuhamasisha wananchi zilikuwa za lugha ya Kiswahili na kukipa Kiswahili dhima mpya ya kuwa alama ya Umoja, Uzalendo, Utanganyika na Uhuru.
3.1.2 Kenya: Nchini Kenya Kiswahili ni lugha ya taifa.Katiba ya Kenya ya ( 2000) Ibara ya 7(1) imekipa Kiswahili sura mpya ya kuwa lugha rasmi na lugha ya taifa. Kiswahili hufundishwa na kutahiniwa shuleni na vyuoni. Lugha hii inayotumika bungeni na katika kuendesha biashara. Kiswahili ni lugha kuu ya mawasiliano wanapokutana watu wa makabila tofauti. Kiswahili kinatumika katika jeshi na polisi. Ni lugha ya kuendesha kampeni za kisiasa mijini na vijijini. Kiswahili kinatumika katika kuendesha ibada makanisani na miskitini. Vyombo vya habari vinavyotumia Kiswahili nchini Kenya bado ni vingi, kinatumika katika programu kadhaa redioni na kwenye televisheni. Aidha nchini Kenya Kiswahili kinatumiwa sana katika mawasiliano ya mitandao ya kijamii na blogu za watu binafsi.
Tume mbalimbali za elimu nchini Kenya ikiwemo Tume ya Mackay, Tume ya Wamalwa, Tume ya Gacathi miongoni mwa tume nyingine zilipendekeza Kiswahilikitumiwe katika ngazi mbalimbali za elimu. Haya yalifanya Kiswahili kushika kasi nchini Kenya. Aidha marais wa kwanza wa Kenya wote walitilia maana matumizi ya Kiswahili kote nchini.
Kiswahili pia kilitumika kama chombo cha umoja miongoni mwa wakenya na moja ya nyenzo ya kuunganisha watu katika harakati za kudai uhuru.
3.1.3 Uganda: Kiswahili kimeanza kutumika kwa mapana na marefu kutoka 2005. Kiswahili kinafundishwa na kutahiniwa katika viwango mbalimbali vya elimu. Aidha, Chuo kikuu cha Makerere kina Idara ya Kiswahili ambayo hufundisha isimu na fasihi kwa Kiswahili. Kiswahili kimekuwa ndiyo lugha ya mawasiliano ikitumiwa zaidi na askari na pia katika kufanya mawasiliano na wageni kutoka katika nchi jirani za Afrika mashariki.
Kiswahili kinatumika sana katika shughuli za biashara na mawasiliano ya kawaida nchini Uganda.
Kuna waandishi wa vitabu vya Kiswahili na pia wanamuziki nchini Uganda ambao wanatunga nyimbo kwa lugha ya Kiswahili
3.1.4 Burundi: Kiswahili kinatumika sana mashariki ya Burundi. Kiswahili kinafundishwa katika baadhi ya vyuo m.f. chuo cha wanajeshi cha Bujumbura na katikaChuo Kikuu cha Bujumbura. Aidha, Kiswahili hufundishwa katika taasisi za mabwana fedha na taasisi ya mawasiliano ya simu. Kiswahili hutumika pia katika Redio Burundi, Ibyizigiro, Isanganiro na katika televisheni kwa baadhi ya vipindi vyake kama vilehabari, matangazo, vipindi vya utamaduni na mafunzo, na matangazo ya mpira.
3.1.5 Rwanda: Kiswahili kinatumika sokoni na mijini. Lugha ya Kiswahili inafundishwa katika chuo kikuu cha Rwanda. Wapo baadhi ya wananchi wanaojiandikisha kujifunza Kiswahili katika madarasa ya jioni. Rwanda imeanzisha Kiswahili katika mtaala wa taifa na kuongezwa katika orodha ya lugha rasmi. Redio Rwanda kuanzia mwaka 1961 imekuwa na programu za Kiswahili kama vile taarifa ya habari, matangazo ya mpira na salamu za wasikilizaji.
3.2 Nafasi ya Kiswahili katika Nchi nyingine za Afrika
3.2.1 Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo: Kiswahili ni miongoni mwa lugha nne za kitaifa zinazotumiwa nchini humo ikiwa ni pamoja na Kilingala, Kiluba na Kikongo. Kiswahili kimeenea zaidi mashariki mwa nchi hiyo ambako kilifika kutokana na misafara ya biashara ya kutoka Zanzibar na Pwani ya Tanganyika.
3.2.2 Msumbiji: Kiswahili kinatumika kaskazini mwa msumbiji. Katika Chuo cha Mambo ya Afrika ya Kusini hutangaza katika Kiswahili baadhi ya vipindi vyao vya redio
3.2.3 Visiwa vya Komoro: Kiswahili hutumika katika badhi ya vipindi vya redio.
3.2.4 Ghana: Kiswahili kinatumiwa na taasisi k.v. Shirika la Utangazaji la Ghana, Taasisi ya Elimu ya Ghana na Chuo Kikuu cha Ghana.
3.2.5 Zambia: Sehemu za Zambia zilizo mpakani na Tanzania hutumia Kiswahili
3.2.6 Somalia: Kiswahili kinatumika Kusini mwa Somalia lakini hivi karibuni kimeanza kuenea kwingi na kwa haraka sana. Hii ni kutokana na maingiliano ya biashara.
3.2.7 Malawi: Kuna wasemaji kadhaa huko kaskazini mwa Malawi
3.2.8 Afrika Kusini: Chuo kikuu cha Kwazulu Natal kimeanzisha masomo ya BAKiswahili.
3.2.9 Zimbabwe: Lugha ya Kiswahili imepangwa kuwa moja kati ya lugha nne za
kigeni za lazima katika mtaala wa elimu .
3.2.10 Libya: Ni moja kati ya nchi za Afrika iliyo nje ya Afrika Mashariki ambayo imekuwa ikiendeleza Kiswahili kwa muda mrefu kwa kufundisha Kiswahili katika moja ya vyuo vyake vikuu vikongwe, chuo kikuu cha Sebha katika Idara ya Lugha na Stadi za Afrika.
3.3 Kiswahili katika sehemu nyingine za Dunia
Lugha ya Kiswahili imekuwa na umuhimu mkubwa duniani kwa ujumla. Matumizi yake kimataifa ni kama ifuatavyo:
1. Mikutano ya Kimataifa:
- · Kiswahili kinatumika kama lugha ya kazi katika vikao vya Umoja wa Nchi za Afrika (AU) kutoka 2004. Uteuzi wa Kiswahili kuwa lugha ya kazi ulitokana na sababu kwamba hakukuwepo na lugha nyingine za Afrika zinazokidhi viwango vya kimataifa.
- · Umoja wa Nchi huru za Afrika (OAU) uliteua Kiswahili kama moja ya lugha za Kiafrika inayotumiwa katika mikutano yake. Uteuzi wake ulitokana na kikao cha Mawaziri wa Utamaduni 1988. Mawaziri walitoa wazo la kuwa na lugha moja ya Kiafrika itakayotumika pamoja na lugha za kigeni kama vile Kiingereza, Kireno, Kifaransa na Kiarabu. Pendekezo la Mawaziri wa Utamaduni la kukifanya Kiswahili kuwa ni lugha ya Kiafrika na ya tano katika vikao vya OAU ni uamuzi mzuri ambao umekipa Kiswahili hadhi kubwakimataifa. Pendekezo hilo liliridhiwa na wakuu wa nchi katika mkutano wao huko Addis Ababa Ethiopia.
- · Kiswahili kimekubaliwa kutumika katika mikutano ya UNESCO mradi tu kuwepo na mkalimani.
- 1. Idhaa za Kimataifa: Kuna vituo vya redio kutoka nchi mbalimbali duniani ambavyo hurusha matangazo yake kwa lugha ya Kiswahili. Mfano wa idhaa hizo ni kama vile Sauti ya Amerika (Marekani), BBC (Uingereza), Redio Deutche Welle (Ujerumani), Redio France International (Ufaransa), China Radio Inaternational (Uchina), Idhaa ya Kiswahili Redio Japan (Japan), Idhaa ya Kiswahili redio Tehran, Idhaa ya Kiswahili ya Redio ya Umoja wa Mataifa, Idhaa ya Kiswahili ya Redio Cairo (Misri), Idhaa ya Kiswahili Iran, Redio Sudani, Redio Vatican, Redio India, Redio ya Korea Kusini, Redio Moscow Inaternational (Urusi).
- 2. Vyuo vinavyofundisha Kiswahili: Duniani kuna nchi mbalimbali ambazo zimeanzisha programu ya somo la Kiswahili katika vyuo vyake vikuuu au kwenye taasisi zake za lugha za kigeni. Miongoni mwake ni:
- (i) Marekani: Kuna vyuo na vituo mbalimbali vinavyofundisha Kiswahili ikiwa ni pamoja na: Chuo Kikuu cha Boston (The African Studies Centre), Chuo Kikuu cha Cornel (Cornell University’s AfricanaStudies and Research Centre), Chuo Kikuu cha Havard (Departiment of African and African American Studies), Chuo Kikuu cha Howard (African Studies Departiment), Chuo Kikuu cha Indiana, Chuo Kikuu cha Michigan, Chuo Kikuu cha Ohio (African –American and AfricanStudies), Chuo Kikuu cha Ohio (Centre for African Studies), Chuo Kikuu cha Stanford, Chuo Kikuu cha Wiscounsin – Madison, Chuo Kikuu cha Pennslvania (Kituo cha Stadi za Lugha za Kiafrika), Chuo Kikuu cha Ilinois (Kituo cha Stadi za Lugha za Kiafrika).
- (ii) Uchina: Kuna vyuo vikuu vitatu nchini Uchina vinavyofundisha Kiswahili ambavyo ni chuo kikuu cha mawasiliano ya habari cha China, Chuo kikuuu cha lugha za kigeni cha Beijing na chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Tianjin.
- (iii) Ujerumani: Vyuo vikuu vinavyofundisha Kiswahili ni pamoja na Humburg, Berlin, Cologne na Leipzig.
- (iv) Uingereza: Kiswahili kinafundishwa katika Chuo Kikuu cha London (School of Oriental African Studies- SOAS).
- (v) Korea Kaskazini: Kiswahili kinafundishwa Chuo Kikuu cha Hankuk.
- (vi) Japani: Kiswahili kinafundishwa katika Chuo kikuu cha Osaka.
- (vii) Ufaransa: Chuo cha INALCO
3. Programu mbalimbali za kompyuta zinazotumia Lugha ya Kiswahili ni pamoja na LINUX operating System, Jambo OpenOffice, Kiolesura Fungasha Kiswahili cha Windows XP, SALAMA ( Swahili Language Manager Program).
4. Mitandao ya simu kama vile Tigo, Vodacom, Airtel, Zantel kwa Tanzania na Safaricom, Orange, Airtel na Yu kwa Kenya inatumia pia Kiswahili.
5. Kiswahili katika uga wa sanaa: Baadhi ya wanamuziki wa kimataifa wametumia maneno ya Kiswahili katika kupeleka ujumbe wa nyimbo zao ikiwa ni pamoja na: marehemu Michael Jackson (Liberian Girl). Lionel Richie, Miriam Makeba (Afrika Kusini), Helmut Lotti (Ubelgiji), Harry Belafonte (Marekani), Rocco Granata (Italia), Peter Seeger (Marekani)miongoni mwa wengine wengi.
6. Kiswahili katika tasnia ya filamu za kimataifa, baadhi ya filamu zinazolenga kutoa maudhui kuhusu Afrika zimekuwa zikitumia maneno kadhaa ya Kiswahili m.f. filamu ya Disney (The Lion king) kuna maneno k.v simba, hakuna matata na rafiki.
7. Kiswahili pia kinatumika kwa wingi sana katika mitandao ya kisasa ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, Instagram, Linkedin na Whatsup. Hali hii inakifanya Kiswahili kuenea kwa kasi mno kote duniani.
Share This :