MASIGNCLEAN101

KIDATO 5 $ 6-KISWAHILI 2- MADA 2 : MAENDELEO YA FASIHI SIMULIZI,

KIDATO 5 $ 6-KISWAHILI 2- MADA 2 : MAENDELEO YA FASIHI SIMULIZI,
citylab
Sunday, 28 October 2018








MADA  2 :MAENDELEO YA FASIHI SIMULIZI

UWASILISHAJI NA UENEZAJI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI

Ni aina ya fasihi ambayo hutumia mdomo katika kuumbwa, kuwasilishwa na kusambazwa kwa wasikilizaji wake.

AU

Ni sanaaa ambayo hutumia mazungumzo na matendo katika kuwasilisha ujumbe uliokusudiwa kwa watazamaji au wasikilizaji.

Mazungumzo hayo huwa katika mfumo wa masimulizi kwa kuumbwa, kutambwa, kuganwa au kutongolewa.Fasihi simulizi hueleza jamii kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa. Fasihi huzungumzia juu ya yale mambo ambayo huzunguka jamii husika na  huathiriwa sambamba na mabadiliko ya jamii na kwa hiyo nayo hubadilika kimaudhui na kifani kufuatia mabadiliko ya mifumo ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii.Fasihi simulizi ni utanzu wa Sanaa ambao hukua na kubadilika kutokana na mabadiliko ya wakati na mifumo ya jamii.

VIPENGELE MUHIMU VYA FASIHI SIMULIZI

(a)          Msimulizi (fanani),Huyu huwa ni mtu ambaye anaitamba hadithi, kuimba wimbo, kusimulia au kutoa vitendawili au methali.

(b)         Wasikilizaji au watazamaji (Hadhira),Hawa ni washiriki katika kutazama au kusikiliza fani ya fasihi simulizi na mara nyingine huwa wanatumiwa na fanani kama wahusika katika kazi yake

(c)Mandhari, Hili ni jukwaa au mahali ambapo tukio la kifasihi (fasihi simulizi) litatendeka.Pahali au mahali hapo yaweza kuwa nyumbani, uwanjani, kuzunguka moto, baharini n.k.

(d)         Tukio/Dhana inayotendeka,Hili huwa ni tendo linalotendeka katika jukwaa la fasihi simulizi. Tendo hili laweza kuwa ni usimulizi wa hadithi, kutega vitendawili, kuimba nyimbo au wimbo au kutoa methali.

SIFA ZA FASIHI SIMULIZI.

Ø Fasihi simulizi hushirikisha fanani na hadhira katika utendaji kwa wakati mmoja.Hii humfanya fanani aweze uonyesha baadhi ya matendo katika usimulizi wake kama vile kutumia viungo vya mwili kwa kuchezesha midomo, kukunja uso, kubinya macho, kuchezesha mabega n.k.

Ø Fasihi simulizi ina sifa ya kuwepo kwa fanani ambaye huweza kusimulia kwa kuimba, kusoma kwa sauti aukubadilisha mtindo wa usimuliaji wake,fanani huweza kufanya yote hayo kama akiona hadhira yake imechoka kusikiliza.Pia ana uwezo wa kuona kama ujumbe wake umeeleweka au la!

Ø Fasihi simulizi zina sifa ya kwenda na wakati na mazingira, tabia hii inatokana na jinsi fasihi simulizi inavyoenea wasikilizaji huwa wengi na hata kama baadhi tanzu za fasihi simulizi zilipitwa na wakati zinaweza kubadilishwa na fanani ili zisadifu mazingira maalumu ya wakati huo.

Ø Fasihi simulizi huzaliwa, hukua, huishi hata kufa hii inasababishwa na mabadiliko yamazingira ambayo hufuata mfumo wa kihistoria wa jamii, mfano kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya kuhifadhi fasihi simulizi katika maandishi ya fasihi simulizi huonekana chapwa kwa sababu ya mambo kama vile miondoko au ngoa, vinakuwa havimo.

Ø Fasihi simulizi ina uwanja maalumu wa kutendea, Fasihi simulizi huwa na sehemu inayochaguliwa kwa ajili ya aina fulani ya fasihi simulizi itakayofanywa na wahusika. mfano tambiko huwa na sehemu maalumu ya kutambikia kama vile sehemu yenye pango,kwenye mti mkubwa kama vile mbuyu, njia panda, makaburini n.k.Hivyo ni wazi kwamba fasihi simulizi inahitaji uwanja wa kutendea yenye kuhusisha vitendo.

Ø Fasihi simulizi ni mali ya jamii nzima.Tanzu zake zote zikishatendwa humilikiwa na jamii kwa pamoja na hii ndiyo inayopatiwa uwezo wa kurithishwa kizazi kimoja hadi kingine.Hivyo huwafikia watu wengi hata wale wasiojua kusoma na kuandika.

MCHANGO WA FASIHI SIMULIZI KATIKA FASIHI ANDISHI

Fasihi simulizi ina mchango mkubwa sana katika fasihi Andishi kifani n kimaudhui

A.Kimaudhui,Dhamira nyingi ambazo ndicho kiini cha maandishi mengi katika  Fasihi Andishi zilikwishajadiliwa  katika fasihi simulizi.Dhamira hizo ni kama vile Mapenzi,Siasa,Matabaka,Uhuru,Ukombozi,Usawa,Unyonge wa mwanamke,Uchawi na Ushirikina n.k Fasihi simulizi haijavumbua dhamira mpya kabisa bali maudhui/dhamira zote za kale.

B. Kifani,Vipengele mbalimbali vya fani ya fasihi simulizi katika kufikisha ujumbe kwa jamii zao.Vipengele hivyo ni;

1.    Muundo,Fasihi simulizi muundo wake ni wa moja kwa moja pia kuna baadhi ya waandishi wa Fasihi Andishi ambao wametumia muundo wa moja kwa moja.Mfano Riwaya ya Kuli(1979) ya Shafi A. Shafi Ametumia muundo wa moja kwa moja.

2Mtindo,Fasihi simulizi hutumia mtindo wa masimulizi pia kuna baadhi ya waandishi wa Fasihi Andishi hutumia mtindo wa masimulizi.Mfano Riwaya yaShida (1975)  ya Balisdya

3. Wahusika,Waandishi wa Fasihi andishi hutumia wahusika wasio binadamu katika kazi zao ambao kwa kawaida hupatikana katika fasihi simulizi tu.MfanoMashetani (1971),Pambo (1975),Adili na Nduguze (1952) Kusadikika (1951) na Kufikirika (1967) wametumia wahusika mashetani ambao hupatikana katika fasihi simulizi tu. Wahusika kama wanyama,majini,mazimwi hupatikana katika fasihi simulizi tu.

 4. Matumizi ya hadithi ndani ya hadithi,hapa wahusika husimulia hadithi mbali mbali katika fasihi andishi .Hawa husimuliana hadithi za kimapokeo ambapo hadithi ni kipera cha fasihi simulizi.MfanoNjozi iliyopotea (1980),Lina Ubani (1984), Mashetani (1971)

5 . Matumizi ya mtambaji hasa katika tamthiliya,Waandishi wengi wa tamthiliya wametumia mbinu ya utambaji ambapo wanakuwa na mtambaji anayetamba hadithi fulani.Mfano,  Lina Ubani (1984),Nguzo mama (1980),Pambo (1975)

6.Matumizi ya mianzo ya hadithi za Fasihi simulizi,Mfano tamthiliya ya Jogoo kijijini na ngao ya jadi(1970) Kilio Chetu (1995) ,Kivuli kinaishi (1990),Riwaya hizi zimetumia mianzo maalum ya fasihi simulizi mfano paukwa……,pakawa.

7. Matumizi ya Semi mbali mbali,Fasihi  andishi hutumia semi mbalimbali ambazo ni ni tanzu za fasihi simulizi.Semi ambazo hutumiwa sana ni misemo,nahau,methali,tamathali ,vitendawili na tanzu nyingine

8. Matumizi ya Ushauri na nyimbo,Waandishi wengi hutumia sana nyimbo katika kazi zao ili kuzipa mvuto,mfano Riwaya yaNjozi iliyopotea(1980),tamthiliya ya Kilio chetu wametumia sana nyimbo katika kufikisha ujumbe kwa jamii husika.

   MADA NDOGO-1;  UWASILISHAJI NA UENEZAJI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI

(a)         UWASILISHAJI WA FASIHI SIMULIZI

Uwasilishaji hutumiwa kuelezea njia au mtindo unaotumiwa kufanya kazi ya kifasihi iwafikie walengwa .Mfano uwasilishaji wa maigizo ni kutendwa kwake jukwaani mbali ya hadhira ya watazamaji.Tangu zamani, uzalishaji wa tanzu za mbalimbali za fasihi simulizi huwasilishwa kwa masimulizi ya mdomo na matendo.Fasihi simulizi hubuni hadithi, nyimbo, methali n.k. zinazobaini hisia zao mbalimbali kuhusu maisha na mazingira yao.Fasihi simulizi pia inaweza kuzungumzia historia ya watu wa jumuiya Fulani itikadi zao na mambo mengine mengi wanayoyathamini katika kuishi kwa pamoja.

Kwa kuwa fasihi simulizi haiandikwi kuhifadhiwa kwake kunategemea kurithishana kwa mdomo kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia hii kizazi kimoja kinaweza kurithisha kizazi kingine yale mambo muhimu ambayo kinataka yaendelee katika jamii hiyo mambo ambayo yamefungamana na mazingira yao maisha yao utamaduni wao na itikadi zao.

(b)UENEZAJI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI

UENEZAJI:

 Hutumiwa kueleza uhusianokati ya hadithi na jamii mbali mbali.Nadharia hii  huonyesha kuwa inawezekana kuwa jamii zinazohusika ziliingiliana kihistoria au kutokana na ukaribu wao wa kijiografia n zilihusiana kihistoria. kuingiliana huku kunaweza kuwa msingi wa kuwako kwa hadithi zinazosimuliwa ambazo zinafanana katika jamii mbalimbali.

Mfano;utenzi wa Fumo Liyongo unapatikana katika jamii kadhaa za pwani ya Kenya kama waswahili, wapokomo, wabajuni n.k. Inawezekana kuwa kupatikana huku ni tokeo la ueneaji hasa kwa kuwa hizi ni jamii zinazokaribiana kijiografia za zilizohusiana kihistoriau

SABABU ZA KUENEA KWA FASIHI SIMULIZI.

a)   Kuanzishwa kwa vikundi vya Sanaa na muziki,Vikundi mbalimbali vya Sanaa na muziki vilianzishwa ambavyo kazi yake ni kuendeleza tanzu mbalimbali za fasihi simulizi hapa nchini.Vikundi vya Sanaa za maonyesho, Vikundi vya taarabu na muziki mfano, Ottu Jazz Band,Kilimanjro orchestra,Kilwa Band n.k vinafanya kazi kubwa ya kueneza na kuendeleza fasihi simulizi hapa nchini.

b)  Muingiliano na fasihi andishi,Kuenea kwa kazi ya fasihi simulizi kwa asili ni kwa mdomo na masikio yaani usimulizi, hata hivyo maendeleo ya watu yamefanya baadhi ya kazi za fasihi simulizi zienee kwa maandishi.Maandishi ni jitihada za kuhifadhi kazi ya fasihi simulizi na kuifikisha mahali ili ikatambuliwe au isimuliwe.Hadithi mbalimbali kama vileHekaya za Abunuasi (1915),Hadithi za Esopo (1890),Fasihi simulizi ya mtanzania.Hadithi (1977) ,Hizi zote zimehifadhiwa na kuenezwa kwa maandishi.

Fasihi andishi inatumia vipengele mbalimbali vya fasihi simulizi katika uandishi wake na hivyo kuviendeleza. vipengele hivyo kama vile ,Matumizi ya semi mbalimbali,Matumizi ya nyimbo,Matumizi ya hadithi ndani ya hadithi,Matumizi ya mianzo na mishilizo ya hadithi za fasihi simulizi,Matumizi ya majigambo, utani n.k.

Kwa sasa methali, vitendawili, nahau, vimewekwa katika maandishi kwa ajili ya kumbukumbu za baadaye na hivyo vinaenezwa kwa njia ya maandishi.

c)    Ufundishaji shuleni na vyuoni,mfumo wa Elimu nchini nao umesaidia kueneza fasihi simulizi kwa kiasi kikubwa hapa nchini kwa sasa fasihi simulizi ni somo linalofundishwa toka darasa la kwanza hadi ngazi za juu (chuo kikuu).Vile vile kuna vyuo hapa nchini vinavyofundisha baadhi ya tanzu mbalimbali za fasihi simulizi kama vile Sanaa za maonyesho na muziki. Mfano chuo cha Bagamoyo, Butimba, Nyegezi na chuo kikuu cha Dar-es-salaam.

d)  Mabadiliko ya kiteknolojia,Kutokana na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kwa sasa fasihi simulizi inaenezwa kwa vyombo vya habari kama vile kaseti, redio, video, luninga, mitandao ya kijamii n.k.Mfano Redio Tanzania (TBC) kupitia kipindi chake cha “Mama na Mwana” “Watoto Wetu” vimesaidia sana kueneza fasihi simulizi hapa nchini Tanzania. Luninga nazo zimesaidia sana kueneza fasihi simulizi nchini kupitia vipindi mbalimbali vya michezo ya kuigiza.Hivyo mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia hayawezi kuwa fasihi simulizi

E)Mwingiliano wa mataifa mengine.Katika mwingiliano muziki umesaidia sana kukuza fasihi simulizi.Hali hii imesaidia kuleta muziki wa kizazi kipya (muziki wa kufoka foka) pamoja na Rege  vijana wa kizazi kipya wamechota miundo na mitindo ya muziki kutoka nje na kuendeleza muziki wao ingawa madhui bado wanajadili yale yale yaliyojadiliwa na wanamuziki wa zamani.Matumizi ya fasihi simulizi katika Sayansi na Teknolojia yamesaidia sana kuenea kwa fasihi simulizi kwani fasihi simulizi inapata hadhira kubwa kwa wakati mmoja lakini hadhira hiyo haionani ana kwa ana na fanani wao kwa kutumia vyombo hivyo vya Sayansi na Teknolojia.

ATHARI ZA SAYANSI NA TEKNOLOJIA KATIKA UWASILISHAJI NA UENEZAJI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI

Mwanzo fasihi simulizi iliwasilishwa na kuenezwa kwa njia ya masimulizi ya mdomo hivyo fanani na hadhira walionana ana kwa ana wakati wa uwasilishaji lakini zama hizi za Sayansi na Teknolojia, uwasilishaji na uenezaji unatumia vyombo vya habari kama vile redio, video, televisheni, kanda kunasia sauti, mtandao na hata kompyuta, mara nyingi hasa hadhira haiwi ana kwa ana na fanani hutokea hadhira ikawa inaangalia luninga au sinema au tamthiliya jukwaani kwenye mazingira kama hayo si rahisi hadhira kushiriki kikamilifu katika utendaji.Kutokana na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia fasihi inaathiriwa katika vipengele vifuatavyo:-

·       Uwasilishaji. Mwanzoni fasihi simulizi iliwasilishwa kwa njia ya masimulizi ya mdomo hivyo fanani na hadhira walikuwa wanaonana ana kwa ana wakati wa uwasilishaji lakini katika kipindi hiki cha sayansi na teknolojia, uwasilishaji wa fasihi  simulizi unatumia vyombo kama, vile redio, luninga, video, kanda, mtandao na hata kompyuta na sio lazima msanii awepo.

·       Uhifadhi, kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia sasa fasihi simulizi inaweza kuhifadhiwa vizuri Zaidi kuliko inavyofikiriwa na wanamapokeo  kwani leo hii fasihi simulizi inaweza kuwekwa katika mkanda wa kompyuta (flash disc) CD, DVD, Maandishi n.k na ikaendelea kuwepo kwa miaka mingi sawa sawa na fasihi andishi hata zaidi.Kwa upande wa video na DVD, uhifadhi wake huendelea kuonyesha vitendo na sauti huweza kudumu hata zaidi ya maandishi.

·       Wakati na mahali, zamani fasihi simulizi ilifanyika sana saa za jioni, kando ya moto au barazani. Aidha kwa vile fasihi simulizi hutolewa redioni inaweza kusimuliwa wakati wowote na mahali popote ambapo kipindi kinasikika na kwa saa na wakati huo. Majumbani, mijini watoto hawazunguki moto tena, bali husubiri wakati kipindi kinaporushwa kwa siku maalumu na wanaizunguka luninga au redio.

·       Hadhira au ushirikishwaji wa hadhira, zamani hadhira ya fasihi simulizi ilikuwa inaonana ana kwa ana na fanani wake wakati wa uwasilishaji wake. Hadhira iliweza kuchangia kazi ya fasihi hiyo na hata kuathiri uumbwaji wake, ikaitwa hadhira tende. Lakini katika muktadha wa maendeleo ya  sayansi si lazima fanani na hadhira waonane ana kwa ana .

MADA NDOGO-2 ;UHIFADHI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI

Kwa sasa fasihi simulizi inaweza kukusanywa na kuhifadhiwa kwa njia zifuatazo:-

Ø Kichwa,uhifadhi wa fasihi simulizi ni katika vichwa vya watu kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Jambo hili limekuwa likifanyika kwa muda mrefu sana.Hivyo kutokana na kuhifadhiwa katika vichwa ndio maana fasihi simulizi imekuwa ikirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine.

Ø Maandishi, Tangu maandishi yagunduliwe baadhi ya kazi za fasihi simulizi zimekuwa zikihifadhiwa kwenye maandishi kwa ajili ya kumbukumbu ya baadaye. Kazi za fasihi simulizi zikihifadhiwa katika maandishi inaweza kufanya watu wasijue ni simulizi au andishi. Hata hivyo vidokezo kadhaa husaidiakujua  kazi za fasihi simulizi kama vile kuwa na mianzo maalum,mfano  “Paukwaa!  Pakawa! Au hadithi…….hadithi njoo” n.k. Aghalabu fasihi simulizi huwa na mtiririko(muundo) wa moja kwa moja usio na urejeshi.

Ø Kanda za kunasia sauti (tepu rekoda),Hii ni njia moja wapo inayotumika kuhifadhi tanzu mbali mbali za fasihi simulizi. Kanda hizo hushika sauti pamoja na vidokezo vyake, kwa hiyo wasikilizaji ili wapate wanachokitaka lazima wanunue kanda hizo.

Ø Kanda za video, luninga na filamu z sinema CD, DVD na Kompyuta/Tanakilishi.Mtandao, picha za video hurekodi sura na sauti,Picha hizo hutembea na kuonyeshwa kwenye skirini ya video na lunnga. Picha za sinema hupigwa kwa aina maalumu za kamera ambazo hupiga picha za mfululizo katika utepe maalumu. Picha hizo huonyeshwa kwa mashine na huonekana  zinatembea, kamera nyingi za sinema za siku hizi zina mitambo ya kurekodi sauti pia. Hivyo kwa kutumia filamu za sinema na video tunaweza kuhifadhi na kuonyesha kazi za fasihi simulizi.

ATHARI ZA MBINU MBALI MBALI ZA UHIFADHI WA FASIHI SIMULIZI

KICHWANI

Uhifadhi wa kazi za fasihi simulizi kichwani una matatizo yafuatayo:-

·       Kumbukumbu za akili zinaweza kupungua au kufifia au fanani kufa kabisa. Hali hii ikitokea fasihi simulizi hupotea.

·       Mtu anayehifadhi kichwani anaweza kubadilisha mambo muhimu katika simulizi na hivyo kugeuza kiini cha masimulizi hayo.

·       Kutokana na mazingira pamoja na mabadiliko kuna tatizo la kupata watu wanaoweza kuhifadhi kazi hiyo.

       MAANDISHI

              Uhifadhi kwa kutumia maandishi una matatizo yafuatayo:-

Ø Baadhi ya  mambo  hayawezi kuhifadhiwa katika maandishi. Mambo hayo ni yale yanayohusianana utendaji, sauti, vitendo, toni, kuimba, muziki n.k. Matokeo ya kukosekana kwa vitu hivi ni kwamba ladha au athari ya kazi inayowasilishwa hupungua.

Ø Kukosa  sauti kwa hiyo msomaji anapaswa atie sauti na mahadhi yake mwenyewe.Shughuli hii inaweza kuharibu au kufanya kazi ya fasihi ipungue ubora wake.

Ø Hakuna ushirikishwaji kati ya fanani na hadhira,kwa hiyo hadhira inashiriki kwa kuona maandishi.

Ø Haibadiliki kulingana na wakati na mazingira. Hivyo huweza kudumu katika hali ile ile kwa muda mrefu kama ilivyo fasihi andishi.

Ø Inakuwa ya ubaguzi au watu wachacheyaani wale wanaojua kusoma na kuandika. Wale wasiojua kusoma na kuandika itawawia vigumu kuelewa fasihi hiyo iliyoko katika maandishi.

Ø Ni gharama kubwa,kuhifadhi masimulizi katika maandishi, hii ni kwasababu uandishi hutumia kalamu na karatasi. Hivyo hapa zinahitajika pesa za kununulia kalamu na karatasi na gharama za uchapaji.

KANDA ZA KUNASIA SAUTI

 Uhifadhi kwa kutumia maandishi una matatizo yafuatayo:-

Ø Kanda za kunasia sauti husikika sauti tuMatendo hayawezi kushikwa na hii kuathiri tena uhifadhi na utoaji wa kazi za fasihi simulizi.

Ø Hakuna ushirikishwaji wa hadhirakwani fanani na hadhira hawaonani ana kwa ana kwa hiyo hadhira inashiriki kwa kusikiliza kanda tu, sikio huathirika lakini jicho halioni.

Ø Ni gharama, kuhifadhi fasihi simulizi kwa njia hii kwani kununua tepurekoda pamoja na kanda zenyewe, betri, spea hupatikana kwa shida na kwa bei ghali licha ya hiyo si wote wenye uwezo wa kununua tepurekoda hivyo ni watu wachache sana wenye uwezo wa kuhifadhi fasih simulizi kwa kutumia chombo hiki.

Ø Haitabadilika kulingana na wakati au mahitaji ya hadhira, Huweza kudumu katika hali ile ile kwa muda mrefu kama ilivyo fasihi andishi.

KANDA ZA VIDEO, LUNINGA, FILAMU ZA SINEMA, CD, DVD, VCD NA KOMPYUTA

Njia hii ina matatizo yafuatayo:-

Upungufu wa ushirikishwaji wa hadhira,Hadhira haiwezi kushiriki ila inasaidia kufanya fasihi simulizi kupata hadhira kubwa ingawa hadhira hiyo haionani ana kwa ana na fanani wao.Kanda hizo huwa zinatazamwa na watu wengi hivyo kupata hadhira wengi kwa wakati mmoja ambao hawawasiliani na fanani wao.

Ni gharama,kwani vitu hivyo vinahitaji pesa nyingi za kununulia vifaa hivyo ambapo ni  watu wachache wenye uwezo wa kununua vifaa hivyo.

Haibadiliki kulingana na mahitaji ya jamii au hadhira au wakati,Huweza kudumu katika hali ile ile kwa muda mrefu kama ilivyo fasihi andishi

Vifaa hivyo vinahitaji mahali pazuri ambapo panaweza kutunza vyombo hivyo kwa muda mrefu, endapo havitahifadhiwa  hivyo kuna hatari ya kupoteza kilichohifadhiwa katika vyombo hivi.

 MADA NDOGO-3; KUHAKIKI KAZI ZA FASIHI SIMULIZI.

Kazi za fasihi simulizi zinaweza kupimwa na kuonekana kama zinafaa au hazifai. Kazi hizi hupimwa kwa kuzingatia uhusiano wake na hali halisi ya jamii.Katika upimaji  vipengele vya fasihi simulizi huangaliwa  jinsi vilivyotumika.Upimaji wa ubora wa kazi ya fasihi simulizi hujumuisha umuhimu wa mambo yaliyosemwa katika jamii inayohusika au namna mambo hayo yanayosemwa Hivyo mhakiki atajiuliza maswali kama:-

Ø Ujumbe utolewao hapa ni wa kweli na una manufaa au la!

Ø Je maadili yatolewayo hapa yanalingana na wakati tulionao?

Ø Je nahau, misemo, methali na tamathali za semi zinalingana na jambo linalosemwa au la!

Ø Je mtiririko wa matukio unasaidia msikilizaji kuelewa kisa au unamchanganya?

Maswali ya namna hiyo yanamsaidia mhakiki kuelewa ubora wa kazi ya fasihi simulizi.Pia yaweza kutumiwa na mtunzi wa kazi ya fasihi simulizi ili kurekebisha kazi yake na kuifanya iwe bora Zaidi.

FANI KATIKA FASIHI SIMULIZI

FANI

Fani ni ustadi au ubingwa au mbinu ambazo msanii wa kazi ya fasihi hutumia katika kuwasilisha ujumbe wake kwa hadhira yake.

AU

 Fani ni Sanaa na jumla ya vipengele vya lugha vilivyowekwa katika mpangilio mahususi ili kutoa  maana fulani kwa hadhira.

VIPENGELE VYA FANI

1.Tukio,Katika tanzu za fasihi simulizi mara nyingi ni lazima pawe na jambo au tukio ambalo huchukuliwa kama kiini au chanzo cha utanzu utakaohusishwa fani au utanzu unaotumiwa na msanii hauibuki tu hivi hivi.Tukio huwa ndio kishawishi cha fanani wa fasihi simulizi .Mfano: Nyimbo za unyago huibuka katika mazingira yake, methali za kutuliza zaweza kutumiwa pale ambapo pana majonzi ya aina fulani, kwa hiyo ni lazima pawe na tukio ambalo litachukua chemichemi ya utanzu utakaotumiwa na fanani kuwasilisha ujumbe wake kwa hadhira.

2.Mazingira/mandhari,Mazingira ni pale ambapo matukio ya fasihi simulizi yaliibuka ama yalitokea.Ufundi wa kuchora mazingira unatoa picha halisi, picha inayoonekana waziwazi juu ya mazingira yaliyohusika.Fasihi simulizi hutegemea sana muktadha au mazingira maalumu hivyo tungo za fasihi simulizi huwa zimejikita katika utamaduni wa jamii zinamoibukia vifaa ambavyo vinatumika katika fasihi simulizi vinategemea mazingira yanayohusika, mfano msanii anapodhaminia kutoa picha ya kuogofya anatumia mazingira ambayo yanaogofya kama vile mazingira ya misituni na wahusika kama majitu ili kuleta dhana ya hofu katika mazingira yake.

3.Muundo,Katika fasihi simulizi muundo ni mpangilio na mtiririko wa kazi ya fasihi simulizi kwa upande wa visa na matukio.Katika muundo kinachozingatiwa ni  jinsi fanani alivyofuma na kuunda hata alivyounganisha tukio moja na lingine kimoja na kingine, wazo na wazo, ubeti na ubeti na mstari wa beti na mwingine.Kuna miundo mbalimali katika tanzu  mbalimbali za fasihi simulizi, kama vile muundo wa moja kwa moja na kuna muundo changamano,pia upande wa ushairi

Katika mashairi kuna miundo mbalimbali ambayo hutumiwa kuainisha mashairi kwa kufuata idadi ya mistari katika kila ubeti, miundo hii ndiyo hutupa mashairi ya tarbia, tathilitha, takhmisa na n.k.Katika hadithi na hata katika tamthiliya waweza kuwa na muundo ambao fanani ameanza kutokamwanzo akaenda katikati na baadae kumalizia kisa chake aina hii ya muundo unaitwa mtiririkoshanga.Mtirirko wa namna hii hujengwa kwa kutumia visa au vitukio mbalimbali na vinaweza kuongezwa na kupunguzwa bila kupoteza maana ya hadithi au tamthiliya.

1.   Mtindo,Katika kazi ya fasihi mtindo ni ile namna ambayo msanii hutunga kazi yake na kuipa sura ambayo kifani na kimaudhui huainisha kanuni au kaida zilizofuatwa kama zilizopo  ni za kipekee. Mtindo ni upangaji wa fani na maudhui katika kazi ya fasihi kwa njia ambayo hatimaye huonyesha nafsi na labda upekee wa mtunzi wa kazi hiyo.

Katika  tamthiliya na riwaya  katika mtindo kinachotazamwa ni matumizi ya nafsi,matumizi ya monolojia,masimulizi na dayalojia,matumizi ya hadithi ndani ya hadithi,matumizi ya barua n.k

 Upande wa mashairi kuna mitindo mbalimbali kama vile Mtindo wa Pindu,mtindo wa kuhoji,mtindo wa beti kubadilishana vina,mtindo wa kidato n.k na shairi linaweza kuwa la vina na mizani au la kisasa ambalo halifuati kanuni za urari wa vina na mizani.

2.   Matumizi ya lugha.

Ni kipengele muhimu cha fani ya fasihi, lugha ndiyo malighafi ya fasihi.Lugha inayotumika katika kazi ya fasihi ni lugha ya kisanaa inayopambwa na inayokusudiwa kuibua hisia fulani kwa hadhira yake.Inaweza kuathiri moyo ya hadhira na kulingana na jinsi inavyotumiwa kwa lengo la kuchekesha, kukejeli, kubeza, kuchokoza, kutia hamasa au kushawishi

     ‘’ Fani lazima iwe na utanashati na ulimbwende wa kipekee wenye mvuto na mnato wa kuteka na kusisimua hisi za wasikilizaji wasomaji au watazamaji’’(khatibu 1981:16)

Matumizi ya lugha fasaha, uteuzi wa misamiati na matumizi ya misemo na methali zinazosadifu mazingira ya jaini inayohusika kufanya kazi hiyo ya fasihi simulizi kuwa sumaku ya kuvutia msomaji, msikilizaji au mtazamaji.Tamathali za semi za aina mbalimbali hutumika kujenga picha mfano ya tamathali za semi ni kama vile sitiari, tashihisi, kejeli, kijembe,tabaini, tuniaba, tashibihan.k.Taswira ni lugha ambayo huchora picha za watu, vitu au mahali kwa kutumia ishara katika taswira unaweza kubainisha maelezo ambayo jinsi yanavypangwa na msanii huweza kufanya hadhira zipate aina mbalimbali za hisi za kunusa, kusikia, kuona na kugusa.Mara nyingi hutumiwa na wasanii ili kunasa hisia zao kwa hadhira.Hivyo wasanii hutumia maneno ambayo huumba picha kamili ya kitu, hali, wazo, dhana au uzoefu fulani wa jamii inayohusika.Mara nyingi matumizi ya picha huenda sambamba na ishara mbalimbali ili kuwakilisha vitu, dhana au mawazo mengine.

3.   Upeo

Katika fasihi simulizi upeo ni kama kilele cha kazi yenyewe, kuna upeo wa aina mbili

Upeo wa juu ,ni zile sehemu za kazi hiyo ambazo hutosheleza haja za wasikilizaji au watazamaji. Katika sehemu hii hadhira hupata majibu muhimu ambayo kazi hiyo imechelewesha kwa kutumia taharuki mbinu rejeshi, mtindo wa kiutelezi n.k.Mara nyingi watunzi wa kazi za fasihi huweka kipeo cha juu mwishoni mwa kazi zao  ingawa si lazima kuwa na kipeo kimoja tu wakati mwingine waweza kupata kazi ya fasihi simulizi ambayo haina kipeo kabisa Katika kazi mbalimbali za fasihi wasanii hujenga mgogoro ambao hujtokeza na kukua, jinsi kazi hizo zinavyokua, kipeo cha juu hutokea pale ambapo msanii hujaribu kutoa suluhisho kwa mgogoro uliojengwa katika kazi yake.

Upeo wa chini ,ni sehemu ambayo matatizo yaliyounda kazi ya fasihi yanatatuliwa.Upeo wa chini ni pale ambapo haja na mataajio ya hadhira hayakukidhiwa, katika baadhi ya kazi za fasihi vipeo vya chini hudhihirisha udhaifu wa kazi hiyo lakini katika kazi nyingine upeo wa chini huwa umekusudiwa hivyo na mtunzi.Hali hii ya pili hujitokeza hasa katika kazi ya fasihi ambayo upeo wa chini hutumiwa kwa lengo la kushangaza hadhira.

4.   UCHESHI KATIKA KAZI ZA FASIHI

Ucheshi ni kipengele muhimu cha kifani katika kazi ya fasihi hasa fasihi simulizi.Ucheshi ni mbinu ya kifani ambayo watunzi hutumia katika kazi zao za fasihi kwa lengo la kuchekesha na kuburudisha hadhira na kuondolea uchovu.

Wasanii mbalimbali hutumia mbinu tofautitofauti kuleta vichekesho katika kazi zao.Baadhi yao hutumia vitendawili ili kujenga, kejeli, dhihaka, n.k. vichekesho pia huweza kutumiwa ili kujenga maudhui.

5.   WAHUSIKA.

Ni viumbe ambavyo hutumiwa na wasanii katika mtiririko wa matukio kuelezea visa vyake.Wahusika wanaweza kuwa watu, miti, wadudu, mizimu, misitu na wanyama.Wahusika huwa ni viumbe ambavyo vinatenda na kutendewa wanatumwa na msanii kusimamia hali mbalimbali za binadamu katika jamii wanamoishi.

Hawa ndio uti wa mgongo wa fani ya fasihi simulizi, Bila wahusika mtiririko wa matukio au visa hukosa pahali pa kujishikiilia.Wahusika si viumbe maalumu wa mtunzi kwa vile ndiyo wanaotumia kutoa picha au kuwasilisha mawazo na fikra zake kwa jamii inayowakilishwa na wahusika hao.Katika Fasihi simulizi  wahusika wanaweza kuwa binadamu ,wanyama,au vitu fulani vilivyopewa fursa ya mandhari na kauli kama binadamu.

VIPENGELE VYA MAUDHUI KATIKA FASIHI SIMULIZI

Ø MAUDHUI

Ni jumla ya mambo yote yanayosemwa na msimuliaji au mwandishi katika kazi yake.Vipengele vya maudhui au umbo la ndani la kazi ya fasihi ni kama vile

Ø Dhamira, Ni kusudio la mtunzi wa kazi ya fasihi.Kazi ya fasihi  inaweza kuwa na dhamira kuu pamoja na dhamira ndogo ndogo.Ubainishaji wa dhamira hufanywa na hadhira,hivyo dhamira hufahamika kutokana na fasili za wasikilizaji au wsomi wa kazi ya fasihi.

Ø Ujumbe: Ili dhamira ya mtunzi itimie, msanii hutoa taarifa fulani fulani kwa hadhira yake.Taarifa hizo huitwa ujumbe. Ujumbe unaweza kutamkwa wazi au kwa uficho. Kwa mfano methali ya “Asiyesikia la mkuu huvunjika guu”  ina ujumbe huu ukidharau maonyo ya wakubwa utapatamatatizo,Siku za mwizi ni arobaini ujumbe wa methali hii chenye mwanzo kina mwisho kwa kawaida kazi moja ya fasihi inaweza kuwa na  taarifa Zaidi ya moja.

Ø Mafunzo: Ni mafundisho au nasaha za mtunzi katika kazi ya fasihi.Mafunzo pia huwa na maana kulingana na fasili ya hadhira. Mafunzo humfikirisha msikilizaji au msomaji kwa njia ya ujumbe.Mfano katika ujumbe huu  akaibaakafungwa hapa funzo ni tusiibe wakati mwingine kazi za fasihi inaweza kutoa mafunzo mabaya (maadili) mtunzi anaweza kukusudia hivyo au kutokusudia hivyo.

Ø Migogoro: Hii huelekeza kisa lakini hujizatiti juu ya migogoro ya maisha anayosimulia fanani.Baadhi ya kazi za fasihi huonyesha ukinzano uliopo baina ya makundi ya watu au hali ya aina moja dhidi ya hali nyingine kuna aina nyingi za migogoro lakini Zaidi ni ile ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni au ile ya kibinafsi mfano: matatizo yanayosababishwa na uzembe dhidi ya watetezi wa kazi (viongozi) dhidi ya usasa katika mila na desturi husababisha mgongano wa kiutamaduni.

Ø Falsafa: Ni mafunzo makuu ya msanii (mtunzi) kuhusu maisha. Mawazo haya hutokana na uchanganuzi wa kimantiki na huwa ndio hekima na busara za msanii (mtunzi) huyo.Ni Imani ya mwandishi au fanani katika maisha juu ya utatuzi wa matatizo katika jamii.

UMUHIMU NA UHUSIANO WA FANI NA MAUDHUI KATIKA FASIHI SIMULIZI.

Fani ni jumla ya mambo mengi yanayoijenga kazi ya fasihi.Mambo haya ni kama vile muundo, mtindo, mandhari,wahusika na matumizi ya lugha na maudhui ni jumla ya mawazo au dhamira, msimamo, mtazamo, falsafa na ujumbe katika  kazi ya fasihi.

Kwa ujumla fani na maudhui ni vitu vya muhimu sana katika fasihi simulizi kwa sababu mtunzi hutumia vipengele hivi katika kujenga kazi yake anayotaka kuwasilisha kwa jamii husika.Maudhui ni kila kina kinachosemwa na fani ni namna kinavyosemwa.

Fani na maudhui ni vitu  vinavyohusiana, vinaathiriana,vinategemeana na kukamilishana katika kujenga kazi ya fasihi simulizi na kila kipengele kimo ndani ya kingine

Mudhui hujumuisha viungo mbalimbali vya kazi ya fasihi simulizi na fani ni mbinu za kisanaa zinazotumiwa na msanii ili kuvifanya viungo hivyo viyasawili maisha kwa njia ivutiayo hadhira.kila kigezo (fani na maudhui) kimo ndani ya kingine huku vikishirikiana na kuathiriana katika kujenga au kubomoa kazi ya fasihi simulizi.

MADA NDOGO-4 ; KUTUNGA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI

Utungaji ni uundaji wa mawazo na kuyapanga maneno yakuwasilisha ama kwa njia ya mdomo au kwa njia ya maandishi.Utungaji unweza kutolewa kawa njia mdomo aqu kwa njia ya maandishi.

Mambo ya kuzingatia katika kutunga kazi ya fasihi simulizi.

·       Kuwa na jambo la kueleza (tukio).Mtunzi anapaswa kuwa na jambo ambalo anaona kuwa linasababisha mivutano katika jamii.Jambohilo lazima litoke katika jamii inayohusika na isiwe nje ya jamii hiyo.

·       Kuteua utanzu utakaotumia.Mtunzi  ni vyema kujua ni utanzu upi atakaotumia katika kuwasilisha jambo hilo kwa jamii.Kwa kawaida fasihi simulizi ina tanzu nne ambazo ni hadithi, ushauri, semi na Sanaa za maonyesho (maigizo).

·       Kuteua vipengele vya maudhui, mtunzi anapaswa aangalie nini dhamira yake, kuna ujumbe gani kwa hadhira, hadhira itapata maadili gani na je migogoro ipi na iwasilishwe vipi ili isipotoshe lengo zima la kazi yake.

·       Kuteua kipera kitakachotumika katika uwasilishaji wa kazi yake kwa hadhira, mfano kama mtunzi ameamua kutumia utanzu wa hadithi; hanabudi kuchagua kipera kimoja wapo kati ya ngano, soga, vigano, visasili au tarihi (visakale)

·       Uteuzi wa vipengele vya fani. Baada ya kubaini vipengele vya maudhui, msanii anapaswa aangalie namna atakavyowasilisha maudhui hayo kwa jamii.Hapa atatumia au atashughulika na vipengele vya fani ambavyo atavitumia katika kuwasilisha ujumbe wake.Vipengele hivyo ni muundo, mtindo, wahusika, matumizi ya lugha na mandhari.Sehemu hii ndiyo ambayo mtunzi anatakiwa kutumia ufundi na ubunifu wa hali ya juu ili kazi yake ieleweke, ielimishe na kusisimua hadhira.

Utungaji wa hadithi za fasihi simulizi

Katika kutunga hadithi yoyote, vipengele vifuatavyo vinastahili kuzingatiwa;

Ø Maudhui

Haya ni masuala yanayowasilishwa na hadithi kwa ujumla wake.Katika utungaji wa kipengele cha maudhui tutazingatia mambo yafuatayo:-

a)Dhamira – Hili ni lengo kuu analowasilisha mtunzi kwa hadhira. Dhamira lazima zitokane na jamii inayohusika. Katika dhamira, kuna dhamira kuu na dhamira ndogo ndogo zinazojenga dhamira kuu. Mtunzi wa hadithi ni lazima azingatie kipengele hiki.

b) Ujumbe na maadili – Hadithi lazima iwe na ujumbe fulani kwa hadhira yake. Mtunzi lazima azingatie hilo. Vile vile hadithi lazima itoe maadili fulani kwa jamii na maadili yanayotakiwa kutolewa lazima yaendane na jamii husika pamoja na wakati.

Ø Fani

  Fani ni jumla ya mambo yote yanayofanywa katika kazi za sanaa ili kufanikisha uwasilishaji  wa ujumbe. Katika utungaji wa hadithi mtunzi anatakiwa azingatie vipengele vifuatavyo kifani:-

·       Ploti/visa ,ni mtiririko wa matukio ya hadithi kuanzia mwanzo hadi mwisho. Kila hadithi ina mwanzo – kati – mwisho. Aghalabu hadithi zina ploti moja nyepesi ya moja kwa moja. Mtunzi katika kipengele hiki cha ploti, lazima azingatie hadithi yake itakayokuwa na mwanzo – kati – mwisho.

·       Wahusika ,Hivi ni viumbe vinavyoshiriki katika hadithi. Hadithi huwa na mhusika mmoja mkuu anayehusishwa na matukio makuu katika hadithi nzima. Wahusika ni wachache na huwa bapa (wasiobadilika) . Mtunzi wa hadithi katika kipengele hiki cha wahusika lazima azingatie ubapa wa wahusika wake katika kuwajenga wahusika wake.

·       Mazingira – Katika kipengele hiki, mtunzi anapaswa kuangalia muktadha kijiografia na kuonyesha:-Mazingira ya kijamii yanayojadiliwa,Majukumu ya mhusika mkuu anayoyatekeleza katika jamii/ familia, n.k,Mahali tukio linapotokea (mahali pa kazi pa mhusika – msikitini, kanisani, ofisini, nyumbani, kijijini, mjini, n.k)Mandhari yakichorwa vizuri husaidia kulisukuma gurudumu la wakati na kwapambanua wahusika.

a)   Kilele – Kilele cha hadithi huwa pale suluhisho la maswali ambayo msikilizaji amefanywa ajiulize hupatikana.

b)  Mtindo wa usimulizi – Hadithi nyingi hutumia nafsi ya kwanza au ya tatu. Zingine hutumia chuku maelezo na kutumia takiriri – mambo ambayo mtunzi anatakiwa kuyazingatia wakati wa utunzi wake.

·       Matumizi ya lugha,Katika kutunga kazi za mtunzi anapaswa kutumia lugha yenye mvuto iliyojaa Taharuki,Tamathali za semi  kama vile tashihisi, tashibiha, sitiari, n.k

UTUNGAJI WA  MASHAIRI/TENZI/NGONJERA WA FASIHI SIMULIZI

 Kabla ya kuanza kutunga shairi lolote, mtungaji anawajibika kuvifahamu kwanza vipengele vinavyojenga shairi, vinginevyo utungaji wake utapwaya sana.Vipengele muhimu vinavyojenga shairi ni vya aina mbili: vya kifani na, vya kimaudhui.

Fani           

Shairi lolote lile ni muungano wa fani, maudhui na muktadha.Kwa kawaida, mashairi  hutunga ili kueleza maudhui fulani kutokana na, au kwa ajili ya muktadha fulani. Shabaha hiyo ya mshairi hutimizwa kwa kutumia fani na hudhihirika kifani. Ingawa maudhui hutawala fani kwa maana ya kuwa mtunzi huanza na wazo ambalo hulitafutia fani ya kulielezea, lakini fani vilevile huathiri maudhui hayo, maana maudhui yamo ndani ya fani na hudhihirika kifani. Hivyo tukitaka kutunga shairi sharti kwanza tuviainishe na kuvielewa vipengele vya kifani vitakavyotumika. Vipengele muhimu vya kifani ni lugha, muundo, wahusika na mtindo.

    (a)Lugha,ushairi hutumia lugha yenye mpangilio na maneno maalumu yaliyoteuliwa ili kuwasilisha ujumbe wake. Kwa hiyo, vipengele vya kuzingatia upande wa lugha ni ;Utenzi wa maneno na semi,Mpangilio wa maneno katika sentensi,Matumizi ya picha (Jazanda) na tamathali: Picha (taswira) ni uwakilishaji wa jambo kutumia kauli maneno yanayosawiri picha au hali ya jambo hilo na kuibua hisia au vionjo kuhusu jambo hilo katika akili ya msomaji/msikilizaji. Picha huweza kumfanya msomaji au msikilizaji, katika mawazo yake, aone, asikie aonje, anuse, apende au achukie kile kinachosawiriwa.

  Tamathali ni aina ya picha. Ni ufananisho wa vitu kisanii kwa kusudi maalumu. Baadhi ya tamathali zinazotumika sana ni tashibiha, sitiari, tashihisi, metonomia (kutumia sehemu ya kitu kuwakilisha kitu kamili, au kutumia kitu kidogo kuwakilisha kitu kikubwa kinachohusiana nacho), mubalagha na kejeli.

Picha na tamathali hutumiwa sana na washairi ili kuyasawiri mawazo yao. Baadhi ya picha na tamathali hizo huwa na viwango mbalimbali vya maana na kuhitaji akili pevu na uzoefu kuzifumbua.

(b)Muundo,mashairi ya Kiswahili yana miundo mingi. Baadhi ya vipengele vya kimuundo vinavyotumika zaidi ni mistari,beti,mizani na vina. Urefu wa wa mistari hutofautiana kutegemea mizani ya shairi linalohusika, au kutegemea mtiririko wa wazo/hisia kama ni shairi huria. Urefu wa beti hutegemea idadi ya mistari katika kila ubeti: zipo tungo za utatu(tathlitha),unne(tarbia), utano (takhimisa), n.k.

Kwa kweli miundo inayotokana na mpangilio wa vina na mizani haina idadi, inategemea matakwa na ubunifu wa washairi wanaohusika.

(c)Wahusika,mashairi ya kawaida hayategemei sana wahusika ili kuwasilisha ujumbe wake. Hata hivyo,yapo mashairi ya masimulizi,kwa mfano, tendi, ambayo hutumia wahusika kujenga maudhui yake. Utungaji wa mashairi ya aina hiyo lazima uzingatie pia dhima na taswira ya wahusika hao katika ujenzi wa matukio na maudhui ya utenzi huo.

(d)Mtindo,mtindo ni tabia ya utungaji ambayo humpambanua mtunzi mmoja na mwingine. Mtindo hubainika katika namna mtunzi anavyotumia maneno yake (Kama anaendelea kutumia maneno magumu au rahisi, kuchanganya lugha, kutumia methali, n.k.) Jinsi anavyozipanga semi zake (kama anatumia sentensi fupifupi au ndefu, takiriri (vibwagizo, n.k.), na namna anavyoumba tungo zake. Mtindo wa mtunzi humwezesha msomaji kubainisha upekee na uasilia wa mtunzi huyo,na pia athari za watunzi wengine kwenye usanii wake.

Mambo muhimu ya kuzingatia katika utungaji wa ushairi wa kimapokeo

Hapa yanaingia mashairi ya tenzi za kijadi zenye kufuata kanuni za urari wa mizani na mpangilio wa vina vya mwisho au kati. Katika ushairi wa kimapokeo,kuna mambo ya msingi yanayosemekana kuwa ni uti wa mgongo wa ushairi wa Kiswahili. Kwa mujibu wa wanamapokeo, shairi la Kiswahili lazima liwe na vina, mizani, mstari, ubeti na kituo. Katika utenzi (aina pia ya ushairi wa kimapokeo) kunakuwa na bahari katika mstari wake wa mwisho. Hapa tutaelezea kwa ufupi juu ya vipengele hivyo.

·       Vina, ni silabi za namna moja zinazotokea baada ya kila mizani kadhaa katika mstari wa shairi. Mashairi ya mistari minne ya mizani 16 huwa na vina katika silabi ya 8 na ya 16 katika mistari mitatu ya kwanza. Kwa kawaida, vina vya silabi 16 huwa vya namna moja katika beti zote za shairi zima, na vina vya silabi 8, kwa desturi inayotumika sana, huwa tofauti ubeti na ubeti. Kwa kawaida tuna vina vya kati na mwisho. Mfano:

       

            Kuna utesi uzushi, nchi ina maongezi,

     Pembeni twaona moshi, moshi haujitokezi,

     Shairi kuzinakishi, kugeuza maongezi,

     Mashairi na utenzi, sanaa tusipotoshi.

          Katika ubeti huu,kuna vina vya kati na mwisho ambavyo hufanana.

·       Mizani ,ni jumla ya silabi zilizomo katika kila mstari wa ubeti.katika ushairi, hizi ndizo ziletazo urari wa mapigo, kwani kila mstari unatakiwa uwe na mizani sawa na mistari mingine. Kwa kawaida mashairi ya kimapokeo huwa na mizani 16, sehemu ya kwanza mizani 8 na sehemu ya pili mizani 8.

Mfano

        Ku na      u te si      u zu shi,  n chi      i na ma nge zi

         8     2   3 4  5   6 7    8    9 10           11 12    13 14 15  16

·       Kituo,Huu ni mstari wa mwisho katika kila ubeti wa shairi. Kituo huweza kuwa kimalizio au kiini.Kinakuwa ni kimalizio kinapokuwa kinatumika kama kitu cha kulifunga na kulikamilisha wazo moja katika kila ubeti. Kinakuwa ni kiini kinapokuwa kikitumiwa na kinajitokeza katika kila mwisho wa ubeti na kinataja kwa muhtasari jambo muhimu linalozungumzwa.

·       Muwala (kutosheleza),Muwala ni ile hali ya utoshelevu katika ubeti hadi katika utungo mzima. Yaani kila ubeti uweze kujitosheleza katika maana, lakini wakati huo huo ukawa hausigani na beti nyingine.

·       Ubeti.,Hiki ni kifungu chenye kuleta maana kamili katika jumla ya vifungu vilivyomo katika utungo.

·       Kipande,Hiki ni kisehemu kimojawapo katika visehemu viwili au zaidi vya kila mstari kwa tungo zenye kugawanyika katika sehemu mbili au zaidi katika kila mstari.

 HATUA/Mambo ya kuzingatia katika utungaji wa mashairi

Ø Kuteua maudhui na dhamira

Katika kipengele cha maudhui, mtunzi wa mashairi anatakiwa kuzingatia vipengele vifuatavyo ili aweze kufanikisha lengo lake.

·       Kuweka lengo maalumu – Kabla ya kuanza kutunga hairi lazima ujue nini unataka kueleza. Hapa lazima ujue sababu inayokufanya utake kueleza hayo uliyonayo. Lengo laweza kuwa kupinga mauaji ya albino, ajira kwa watoto au unyanyasaji wa wanawake.

·       Kuteua wazo kuu la shairi – Hili ndilo wazo utakalolikuza na kuliendeleza. Wazo kuu linaweza kuwa “ athari za ugonjwa wa UKIMI” katika jamii. Hivyo mwandishi ataliendeleza wazo hilo kutoka mwanzo hadi mwisho.

·       Kuoanisha dhamira na wakati – Ni muhimu mtunzi wa ushairi kuhakikisha kwamba anazungumzia mambo ambayo anafikiri jamii inayahitaji katika wakati huo. Kwa mfano, leo Tanzania imekabiliwa na matatizo kama vile ugonjwa wa UKIMWI , ajira kwa watoto, mauaji ya albino, madawa ya kulevya, n.k. Haya ndiyo mambo ambayo mtunzi hupata hadhira kubwa. Kama taongea mambo ambayo yako nyuma ya wakati, atakuwa haitendei haki jamii yake kwa kujadili mambo ambayo hayako katika jamii yake kwa wakati uliopo.

·       Kupanga vizuri mawazo yako – Panga mawazo yanayojenga maudhui kimantiki kutegemea uzito, upya, ugumu na umuhimu wake kwa jamii inayohusika.

Ø Kuteua vipengele vya fani

Maudhui pekeehayatoshi kulipa shairi mvuto. Mtunzi ni lazima azingatie fani, yaani mbinu za kisanii anazotumia mtunzi kulipa shairi mvuto. Mbinu hizi ni pamoja na:-

·       Kutumia mitindo inayofaa – Shairi linaweza kuwa la kimapokeo au kisasa. Uteuzi wa mtindo untegemea sana dhamira inayokusudiwa pamoja na lengo alilonalo mtunzi mwenyewe. Kwa mfano, tukio la kihistoria utatumia “utenzi” badala ya “wimbo”, mawaidha fulani huwezi kutumia “utenzi” bali utatumia “ushairi” au “wimbo”.

·       Kutumia miundo inayofaa,Kuamua muundo wa shairi kutategemea idadi ya mistari. Mtunzi anaweza kutumia muundo wa tathnia (mistari miwili), Tathlitha (mistari mitatu), Tarbia (mistari mine), Tkhimisa (mistari mitano) au sabilia (mistari sita na kuendelea). Katika kipengele hiki ni muhimu vile vile mtunzi kuzingatia idadi ya mizani, aina ya vina, vipande, kituo msisitizo, muwala, ubeti na urari. Vitu hivi ni muhimu sana hasa kwa ushairi wa kimapokeo.

·       Uteuzi wa lugha – Ushairi una lugha yake ya tofauti na kazi nyingine. Mtunzi hana budi kutumia lugha yenye sifa zifuatazo:- Lugha ya mkato, -Matumizi ya picha, Matumizi ya tamathali za semi, Matumizi ya methali, misemo, nahau na mbinu nyingine za kisanaa

                    UTUNGAJI WA MAIGIZO YA FASIHI SIMULIZI

Katika utungaji wa maigizo kuna vipengele mbali mbali ambavyo lazima vifuatwe  ili utungaji  ukamilike. Vipengele hivyo ni :-

·       Kuchagua tendo au tukio la kuigiza ,Mtunzi achague matendo yale tu ambayo lazima yatasaidia kujenga wazo lake. Ni lazima jambo hilo liwe uzito au athari fulani kwa jamii. Matukio yanayoweza kuwa kiini cha kutungiwa maigizo ni kama vile ufisadi, malezi ya watoto, unyanyasaji w mwanamke, mauaji ya albino, ujambazi, madhari ya UKIMWI, n.k

·       Kuchagua mahali pa kutenda jambo ,Mahali pa kutenda panaweza kuwa ofisini, nyumbani, barabarani  kwenye basi, mjini, kijijini, n.k.

·       Kuteua mtindo na kuteua jambo la kuigizwa,Hapa mtunzi anaweza kutumia fumbo, vichekesho, tanzia, ramsa (futuhi), n.k. Ni vizuri mtunzi achanganye mbinu ili kutdumisha mvuto.

·       Kupanga hoja zinazojenga maudhui ya igizo,Maudhui hujikita katika migogoro. Masuluhisho ya migogoro hupatikana pale migogoro inapofikia kilele. Kwa mfano, mwanamke anapojikomboa kutokana na manyanyaso ya mwanaume.

·       Kuweka mpangilio wa maonesho,Maonesho ambayo hujumuisha vitendo na hoja  zinazokamilisha sehemu inayobeba maudhui ni muhimu sana. Maonesho yapangwe kwa utaratibu maalumu ili yaweze kufikisha ujumbe kirahisi kwa hadhira. Maonesho yakipangwa ovyo, mvuto wa kazi ya sanaa huwa ovyo pia.

·       Ujengaji wa wahusika-Wahusika wajengwe kutokana na misukosuko ya migongano. Matendo, maneno na mawazo ya wahusika yapate chanzo kutokana na misukumo hiyo. Mtunzi anashauriwa kutumia wahusika tofauti tofauti. Kwa mfano, wazee, vijana, wanawake, wanaume, wanene, wafupi, wembamba, n.k. Ni muhimu pia kwa mtunzi kuwaumba wahusika wake na kuamua mavazi yao na vifaa vingine. Uamuzi huu yafaa ufanywe kwa kuzingatia mazingira.

·       Uteuzi wa maneno – Maneno ya kusema wahusika yanapaswa kuwa yale tu ambao yanajenga tendo. Maneno yanajengwa ili kudhihirisha tendo liwe wazi zaidi. Kuweka maneno mengi hudhoofisha nguvu ya matendo, katika kuleta maana inayokusudiwa kwa vile huwa vigumu hupatanisha maneno hayo na matendo. Kwa hiyo, mtunzi wa maigizo anapaswa kuwapa wahusika wake maneno machache jinsi iwezekanavyo, na tena yale tu ambayo yanaoana na vitendo.

·       Baada  ya yote hayo, mtunzi anawezakuandika maigizo na kuhariri – Ni muhimu kutumia lugha ya kimazungumzo (dayolojia) inayovutia na kuleta taharuki na yenye utamu unaoeleze maadili kwa mnato.

            M  W    I  S  H  O

Share This :
...