MASIGNCLEAN101

Pragmantiki kwa Ujumla katika Kiswahili

Pragmantiki kwa Ujumla katika Kiswahili
citylab
Sunday 29 May 2022
Pragmantiki ni taaluma iliyo na Nadharia. Katika kujibu swali hili tumeweza kuligawa katika sehemu kuu tatu, yaani Utangulizi, ambapo katika utangulizi tutaelezea maana ya Pragmantiki na Nadharia kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali, Pili Kiini, katika kiini tutaelezea Nadharia za Pragmantiki pamoja na mihimili ya Nadharia hizo, pia katika Hitimisho tutaelezea umuhimu wa nadharia za Pragmantiki.
UTANGULIZI
Kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali walioelezea maana ya Pragmantiki na Nadharia kama ifuatavyo;
Massamba (2004) anasema Pragmantiki ni taaluma ya isimu inayojishughulisha na uchunguzi na uchambuzi wa lugha katika mawasiliano. Lengo kuu la taaluma hii ni kuchunguza namna lugha inavyotumiwa na wasemaji wake katika mazingira halisi.
Yule (1996) anafafanua dhana ya Pragmantiki kwa kusema kuwa ni taaluma inayohusu mahusiano yaliyopo kati ya maana ya Lugha na watumiaji wa mambo hayo.
Richmond (2012) anasema kwamba Pragmantiki ni tawi la Lugha linalojihusisha na matumizi ya Lugha kwa kuzingatia muktadha wa wazungumzaji husika. Hivyo Pragmantiki inahusu zaidi mambo mawili ambayo ni;
i/ Matumizi
        ii/ Muktadha.
Hivyo basi, kwa ujumla tunaweza kusema kuwa pragmantiki ni taaluma inayohusiana na matumizi halisi ya lugha katika miktadha tofauti na uelewa wake kama vile malengo hayo.
  Mfano;
 Matumizi ya Lugha katika muktadha wa  hotelini ambapo mtu anaweza kusema,
  i/ Nipe wali kuku.
 ii/ Nipe chai tatu.
Hivyo Muktadha wa Hotelini huweza kufuatwa na wazungumzaji wa lugha.
Pia wataalamu mbalimbali wanaelezea maana ya Nadharia kama ifuatavyo,
Sengo (2009) anaeleza Nadharia kuwa ni wazo kuu, fikra kuu, mwongozo mkuu wa mtu, watu au jamii ya pahala fulani kwa sababu fulani.
Mdee (2011) anaeleza Nadharia kuwa ni mpango wa mawazo uliotungwa ili kueleza jinsi ya kufanya au kutekeleza jambo.
TUKI (2004) wanasema Nadharia ni mawazo, maelezo au mwongozo uliopangwa ili kusaidia kueleza, kutatua au kutekeleza jambo.
Hivyo, Nadharia ni mawazo au maelezo yanayotolewa kuelezea hali fulani.
Mfano;
Chanzo chake, Muundo wake, Utenda kazi wake.
Si kweli kusema kwamba pragmatika ni taaluma isiyo na nadharia bali pragmatika ni taaluma yenye nadharia kama ifuatavyo.
  (i) Nadharia ya isimu jamii ya mtagusano.
Nadharia ya isimu jamii mtangusano ni mkabala wa kiuchanganuzi usemi ulio na chanzo chake katika kutafuta mbinu za kufasiri kile ambacho wahusika wa mawasiliano hudhamiria kuwasilisha kila wanapoongea.
Nadharia hii inatambua kuwa wawasilianaji, kila mara hutegemea maarifa na kusikika huku wakielewana.
Gumperz (1982) anasema, Nadharia hii huwa na mihimili ambayo huiongoza katika utenda kazi wake . Mihimili hiyo ni; 
  i/ Uanuwai kitamaduni.
  ii/ Usuli wa kimawasiliano.
 iii/ Maongezi baina ya wahusika katika miktadha.
 
Mihimili ya Nadharia ya Isimujamii ya mtagusano
i/ Uanuwai kitamaduni.
Dhana hii ya Uanuwai kitamaduni inamaana kuwa kila msemaji anautamaduni wake ambao hutofautiana na wamwenzake. Hali hii hujitokeza kwa sababu mtagusano huhusisha tamaduni zaidi ya moja katika miktadha mbalimbali.
Mfano,
 Muktadha wa kanisani hukutanisha watu wa tamaduni tofauti, hivyo hulazimika kufuata utamaduni wa Muktadha wa kanisani pekee. Mfano katika salami, maongezi
ii/ Usuli wa kiisimujamii.
Usuli huu wa kiisimujami wa kila mhusika katika mawasiliano hujitokeza na kuchangia pakubwa katika usimbaji na usimbuaji wa maana ya mawasiliano.
Katika jamii mawasiliano mara nyingi huwa hayakamiliki na huhitaji msikilizaji kujijazia kile ambacho msemaji anasema au analenga kusema.
Garfinkel (1967) anasema Mjazo huu wa ziada kutoka kwa msikilizaji kunatokana na kuwa na usuli wa kiisimujamii.
Mfano,
Juma: Baba amenituma kwako, anasema unipe (....).
Chizua: Ah!! Baba yako anakichaa, nimemwambia sina. Nikipata nitamletea mwenyewe.
Katika mfano huu tunaona kuwa  "Juma" hakukamilisha kauli yake pengine kwa sababu anaamini kuwa "Chizua" anahabari za kiusuli kuhusu kile ambacho Juma ametumwa na Baba yake.

(ii)  Nadharia ya ushirikiano
Nadharia hii iliasisiwa na H.P Grice(1913-1988) hasa mnamo (1975).Katika maelezo haya tunayatumia maelezo ya Leech (1983) kwa mapana, nadharia hii hueleza kuwa watumiaji wa lugha hujaribu iwezekanavyo kushirikiana pale wanapowasiliana.Hujaribu kutoa habari zote muhimu za kweli, zifaazo na kwa namna inayoeleweka bila ya kutatiza.Ushirikiano huu huwa baina ya mzungumzaji na msikilizaji au(maandishi na msomaji) Grice (1975); anasema kuwa utaratibu wa ushirikiano una kanuni nne muhimu yaani 

     (a) kanuni ya idadi au kiasi.
Kanuni hii inapendekeza kuwa msemaji atoe kiasi  kifaacho Cha habari, aspunguze wala kutoa habari zisizohitajika 
Mfano;Anitha: Frola atakutana na mwanaume leo
            Theresia: Je, mumewe Frola ajua jambo Hilo?
           Anitha: Bila shaka mwanaume atakayekutana  naye ni John mumewe Frola.
Hapa Anitha amevunja kanuni ya idadi kwa kuwa neno mwanaume halitoi maelezo ya kutosha; angetumia neno mumewe hata hivyo hajavunja kanuni ya sifa  kwa kuwa habari anazozitoa ni za kweli

(b) Kanuni ya sifa au ukweli.
Kanuni hii inapendekeza kwanza,habari anazozitoa mzungumzaji ziwe za kweli yaani asiseme kitu anachoamini kuwa si kweli,na pili asiseme jambo ambal hana Ushaidi wa kutosha kulifafanua.Kwa mfano;Baraka ni mlevi wa pombe.
Tunalofahamu ni kwamba si kweli mtu kusema kauli Kama hii ikiwa anajua kwa hakika kuwa Baraka hanywi Wala hakuna ushaidi wowote unaoweza kutumika kuthibitisha dai hili ilivyo ni kwamba tunafaa kutoa kauli kuhusu jambo tulilo na uhakika nalo.

(c) Kanuni ya ufaaji
Kanuni hii husisitiza kuwa wazungumzaji wasitoke nje ya mada.Hapa kanuni hii hutuelekeza kiasi cha kuyaandaa matamshi yetu ili yaafikiane na mahitaji na matarajio ya mazungumzo.katika Hali hii hatutarajiwi kubadilisha gafla wala kuzungimzia yasiyowiana na mada ya mazungumzo.Hivyo taarifa  au kazi tunazozitoa zinafaa kuhusiana na mada ya mazungumzo,wazingatie lile linalozungumzia na kwa njia hii mawasiliano hutokea  hata Kama baadhi ya maneno yataondolewa kwa mfano;
   Amina: Wanafunzi wa shule ya sekondari kibondo wametoroka.
   Cherish: Walipotoroka hapakuwepo na walinzi wakati huo?
Amina: Hilo sijui.....
Neema: ooh yule mwajuma ni mnafika Sana.
Ni wazi kwamba Amina na Cherish wanaelewa kile wanachozungumzia.Lakini Hali ni tofauti na mwenzao Neema ambapo mchango wake hauendani na mada ya wanafunzi kutoka shuleni.Neema katoka nje ya mada kabisa na hivyo kupotosha mawasiliano.Tufahamu kuwa wakati mwingine wasemaja wanaweza kutoa majibu kiumanisho.  Mfano,
     A: Tina yupo?
      B: Nimeona mlango wake upo wazi.
Hapa japo jibu halitolewi moja kwa moja tunaweza kuurejelea muktadha wa mazungumzo haya ambapo tunahusisha na mazungumzo au maingiliano na muktadha w kigali.

(d) Kanuni ya jinsi au namna
Kanuni hii inapendekeza Mambo yafafanuliwe kwa njia iliyodhahili,wazi na isiyokuwa na utata.Kanuni hii inahusu vile jambo linavyosemwa na wala si kile kinachosemwa.Inapendekeza kuwa 
      a, Mambo yasisemwe kwa njia ya mafumbo, mizunguko.
      b, Wazungumzaji wajiepushe na utata
     c, Mambo yasemwe kwa kifupi iwezekanavyo
     d. Mambo yasemwe kwa mpangilio mzuri
Kwa kawaida watumizi lugha huchukulia kuwa utaratibu huu unafuatwa wakati wa mazungumzo.
Kwa mfano.       Mangi; Habari yako Juma,unataka Nini?
                           Juma ; Salama mangi niuzie nyanya,vitunguu,karoti na hoho.
Mazungumzo haya yanaonyesha kwamba, mawasiliano haya Kati ya Mangi na Juma yanazingatia kanuni ya ufaaji kwa sababu Kuna mpangilio sawa, maelezo ni mafupi na yanalenga,hayana utata wowote na hayakutamkwa kwa mafumbo.Kaida hii husisitiza kuwa tunafaa kujikita kwenye mazungumzo ambapo msemaji yeyote(katika uandishi wa kazi ya Sanaa,maandishi) anaweza kusimulia hali, mambo,na matukio yanayotendeka na baadaye hurejea kwenye mada au matukio yanayofanyika wakati uleule wa kuandikwa. 

 ( iii). Nadharia ya matendokauli
Austin(1962)ndiye mwanzilishi na muasisi wa nadharia ya matendo kauli(speech act theory) kisha Searle(1969-1979) akiboresha Nadharia hii kwa kuyaainisha matamko mbalimbali,kauli-tamko,kauli-tendi na tamko tekelezi (locutionary, illocutionary,percutionary). Nadharia hii inaweka wazi masharti ambayo yatimizwe ili matendo kauli yanayolengwa yaweze kutimizwa.Nadharia hii ya matendo kauli hujitokeza katika mazungumzo yanayohusisha wanajamii katika tukio flani la maingiliano.nadharia hii huchukulia kwamba maingiliano ni matukio ya aina fulani ambayo hulenga kutekeleza kauli fulani.Kwa mfano kufahamisha,kusihi,kufurahisha na kuonya.matendo kauli huchukua mikondo mitatu kama ifuatavyo:-

(i) kauli-tamko,hapa tunaangalia uhalisia wa kutoa tamko lenye umbo na maana mahususi,mintarafu ya wasikilizaji,wahusika,katika mazungumzo haya ni matamko halisi yanayotoka kinywani mwa msemaji.
Msemaji hutoa maneno na nahau zingine zenye kusababisha athari flani ,matamko haya hutumia lugha ya moja kwa moja inayotamkwa.
ii) Tamko-tendi,Hili ni tamko linalotolewa na msemaji ambae anaongozwa na malengo mahususi katika muktadha unaofaa kwa mfano toka nje,hapa msemaji atakuwa ametoa amri au agizo kwa msikilizaji ambaye anaweza kuikaidi au kuitii amri hiyoo,hapa tunashuhudia hali halisi ya kusema na kutoa matamko mbalimbali,kwa kawaida tamko lolote hufungamanisha kauli -tamko na kauli-tendi,tamko lolote ni rundo au mfuatano wa sauti zinazosikika na maneno yanayolengwa kwa namna fulani na yanayolengwa kutekeleza jukumu fulani.
iii) Tamko-tekelezi,hii ni kauli tendi ambayo inadhamiria kusababisha athari fulani kwa msikilizaji,kwa mantiki hii hitoshi tu msemaji;-
A: kutamka kuwa anadhamiria kusoma shuleni.
B: umuhimu uwekewa athari inayoendana na kauli au tamko linalohusika ;-shule itafutwe na mtoto huyu ataanza darasa la kwanza,hivyo tamko tekelezi hutuwezesha kufahamu kwamba kauli-tamko na Tamko-tendi huibua matendo kauli yanayotuwezesha kubadili hali flani ya kijamii,kwa Hali hii tamko tendi,huendana na tamko tekelezi mahususi.
(iii) Nadharia ya upole
Leech (1983), anaeleza kwamba nadharia ya upole imejengeka kwenye msingi uliowekwa na nadharia ya ushirikiano ambayo kwa mujibu wa Grice (1975), Ni muhimili mkuu wa maingiliano kwa njia ya mazungumzo. Nadharia ya upole inaeleza kwamba wanaoshiriki mazungumzo hutarajia kuwa wenzao watakuwa tayari kushirikiana nao. Nadharia hii kwa kiasi kikubwa huyatawala mazungumzo kati na baina ya watu na husaidia katika kuimarisha mawasiliano kwa kusababisha mahusiano mema baina ya wasemaji. Katika hali hii watumiaji wa lugha hufungamanisha mikakati mbalimbali kutegemeana na utamaduni, mazingira na muktadha wa maingiliano husika. Kwa kweli miktadha mbalimbali hutofautiana na hali hii hujitokeza kwenye tofauti ya maumbo yanayotumiwa katika kBrown na Levinson (1987), waliikuza nadharia hii ili iwawezeshe wahakiki na wachambuzi wa kiisimu kuelewa mambo ya kimsingi na anuwai katika maingiliano ya ana kwa ana. Dhana ya upole kwa kiasi kikubwa hutofautiana katika jamii mbalimbali. Kwa hali hii, kila mtu huwa mbioni katika kulinda ‘uso wake’ ambapo huhakikisha anadhihirisha nafsi inayopendeza kukumbatiwa na wengine. Hivyo mtu huhakikisha anaonekana na kutambulika na kuonekana vema na wale anaotagusana nao. Kutokana na kuwa kila mtu hupenda kuheshimiwa kama mtu huru aliye na idhini ya kutenda lolote pasi na kulazimishwa, hulazimika kuhakikisha anajiepusha na kauli au matamko yanayoweza kuwavunjia heshima na kuwatia watu kwenye aibu.
Leech (1983), anapendekeza kanuni tatu kuu ambazo zinaweka wazi nadharia ya upole nazo ni kama ifuatavyo÷
a) Kanuni ya hekima, kanuni hii inasisitiza kwamba tunafaa kupunguza hasara kwa wengine huku tukizidisha faida na manufaa yao.
b) Kanuni ya ukarimu, tujipunguzie faida huku tukijizidishia hasara.
c) Kanuni ya staha, tujipunguzie sifa (majisifu) huku tukijilimbikizia utosifa. Vilevile tuwapunguzie wengine utosifa huku tukizidisha sifa zao.
Kanuni hizi huchukuana vizuri na msingi uliowekwa na Goffman (1976) anayesisitiza kuwa wanaoingiliana huhakikisha wanakuza na kuhifadhi hulka na sifa zao. Kanuni hizo zinazokuza upole huendana na kanuni ya ushirikiano iliyowekewa msingi wa nadharia ya ushirikiano iliyokuzwa na Grice (1975, 1989) kwa mujibu huu wanaoshiriki mazungumzo hutarajiwa kuingiliana kistahilifu. Uwezo wa kila muhusika katika maingiliano hayo hutokana na miiko ya kijamii. Kwa kawaida mwanajamii ambaye, anauelewa utamaduni fulani kindakindaki anafahamu barabara miiko inayoandamana na namna ya kuzingatia maumbo yanayojenga kauli za upole. 
Levinson (1987), anaeleza kwamba maumbo yanayoweza kusababisha aibu kwa wanaoshiriki mazungumzo ni pamoja na maombi ( Nipe kalamu yako), amri ( kuja hapa) mapendekezo, lakini pia matamko yanayoweza kuwaaibisha wazungumzaji ni pamoja na ukosoaji, malalamiko, mizozanona kutokubaliana na maelezo yasiyo afiki mada ya mazungumzo. Mfano mtu usiye fahamiana nae na ulietengana nae masafa ya kijamii hawezi kumuuliza mwenzie maswali ya kibinafsi kama vile una watoto wangapi? Pia huwezi kumdunisha, kumshutumu au kumkejeli. Katika kiswahili upole hujitokeza katika maumbo na matamko mbalimbali mfano; Ndugu mpendwa, Shikamoo, Marhaba hujambo. Mifano mingine ni kama vile Shukrani, Karibu, kwaheri na kadhalika.
Cruse (2006), anaeleza katika kudhihirisha upole, wazungumzaji wanafaa kuzidisha sifa inayomkuza na kumkweza msikilizaji kiasi cha kueleweka vizuri na kuwa katika mkabala mzuri na wengine. Aidha msemaji anapaswa kupunguza makali ya sifa yoyote ambayo inaweza kumdhalilisha na kumdunisha msikilizaji. Majivuno na majisifu anayojilimbikizia mtu ni dalili na mfano wa kutokuwa mpole. Ikiwa msemaji anaposhiriki mazungumzo atajidunisha na kujidhalilisha basi atasemwa yeye ni mpole. Dhana ya upole ni tabia au tukio la kiisimu ambalo hufungamanishwa na wasemaji na wasikilizaji katika hali halisi ya kimazungumzo. Upole huu hufungamana na msemaji na yale yanayomtukuza nafsi yake, hali ambayo inaweza kumkasirisha msikilizaji. Kwa hali hii basi maringo, majivuno na majisifu ni namna inayokuza hali ya utoupole yaani hali zinazopunguza staha, heshima na adabu.
(v) Nadharia ya uchanganuzi usemi
Nadharia ya uchanganuzi usemi huchunguza namna ya watumiaji wa lugha huingiliana katika hali halisi ya kimawasiliano. Hapa matamko yanayotolewa na wasemaji huchukuliwa kama vipashio vyenye maana na vinavyobeba taarifa muhimu zinazofahamika kwa wahusika wawili au wengi. Matamko haya huelekea kuandaliwa kitaratibu na kimantiki kulingana na mkakati na mtazamo wa Grice (1975), unaosisitiza uwezekano wa wasemaji kushirikiana na kukubaliana kuhusu namna ya kuyaendesha na kuyakamilisha mazungumzo baina yao. 
    Mtazamo huu hushughulikia wasemaji au utamkaji wa mwanadamu kama tukio lenye kudhihirisha tabia, tajiriba, na malengo ya wasemaji. Hapa tunafaa kuangalia namna watumiaji/wasemaji wa lugha hupokezana zamu, wanapoangalia, wanaposema na namna huhakiki na kukatisha usemi wa wenzao katika mazingira na miktadha halisi ya matumizi ya lugha. Eneo moja linalopewa umuhimu mkubwa katika nadharia hii ninshughuli ya kupokezana zamu na kukatizana zamu. 
     Nadharia hii hubainisha kauli kwamba mazungumzo ni harakati iliyo changamanwa na iliyofungamana na muktadha wa mazungumzo/maingiliano. Aidha mazungumzo yoyote katika muktadha wowote hueleweka kwa kuchunguza azma na malengo ya wanaoshiriki mazungumzo hayo. Heritage (1984), anasema kuwa watu wawili wanaofahamiana wakikutana barabarani au popote mmoja anatarajiwa kumsalimu mwenzake. Akijibu salamu hizo basi atakuwa amedhihirisha hali ya upole na 'urafiki'; vinginevyo, atakuwa amekiuka kaida na taratibu zinazofungamana na nadharia ya uchanganuzi usemi. Kwa ujumla uchanganuzi usemi hudhihirisha ruwaza maalumu zinazotawala mazungumzo; ambapo wanaoyashiriki mazungumzo hayo hubadilishana zamu huku wakipunguza nyufa, mapengo, na upishanaji (Sacks, Schegloff na Jefferson, 1974). Mazungumzo hayo hutawaliwa na kaida zinazoendana na upokezanaji zamu nia ikiwa ni kuyafanikisha maingiliano kati na baina ya wazungumzaji (Schegloff naSacks 1973;Sacks1987).Vivyo hivyo kuna taratibu mbalimbali zinazofungamana na ukarabati wa mazungumzo yenye uwezekano wa kutofaul/kusambaratika(Schegloff,Jefferson na Sacks, 1977;Brown 1997).

(vi) Nadharia ya Diskosi hakikifu changanuzi
Van Dijk (1998) anafafanua diskosi hakikifu changanuzi ( kwa maana ya critical discourse analysis)Kama mtaala unaoshughulikia uchambuzi na uhakiki wa matini ama iliyoandikwa ama iliyosemwa,kwa lengo la kutambua vianzo vya mamlaka,utosawa na amri juu ya upendelevu.Aina hii ya diskosi huchunguza namna hali hizi mbalimbali za mamlaka huhifadhiwa na kuendelezwa katika hali na miktadha mahususi ya kijamii,kisiasa na kihistoria.Diskosi hii huchunguza udhihirikaji wa mamlaka katika asasi na maingiliano mbalimbali(mwalimu na mwanafunzi,Askari na mshukiwa wa uhalifi,daktari na mgonjwa).
   Nadharia ya diskosi hakikifu changanuzi pia inaweza kujitokeza katika taaluma ya fasihi.Diskosi hii pia hushughulikia masuala ya urasimu na harakati za kikazi (Wodak,1996). Fairclough (1993;1995)  anafafanua diskosi hakikifu changanuzi Kama aina ya uhakiki wa diskosi unaolenga kueleza uhusiano usio wa mojaa kwa moja Kati ya Hali na shughuli mbalimbaali za kijamii.katika Hali hii diskosi hakikifu changanuzi hulenga kuchunguza na kuhakiki
(i) Mahusiano ya kimfanyiko yanayojitokeza katika Muktadha mbalimbali,matukio na matini.
(ii) Namna mifanyiko,matukio na matini zinavyokutana na mielekeo ya itikadi inayoendana na mahusiano ya kimamlaka na mashindano ya kimamlaka.
(iii) Miundo mipana ya kijamii na kitamaduni inayobainisha mahusiano ya kimamlaka Kati ya washirika mbalimbali katika jamii.
(iv) Kubaini Mahusiano ya kimamlaka yaaliyofichama ndani  ya jamii kwa minajili ya kukuza maelewano.
Kwa kifupi, diskosi hakikifu changanuzi hulenga kuweka wazi uhusiano Kati ya mifaanyiko ya kidiskosi,ya kijamii,pamoja na Miundo ya kijamii ambayo,kwa kiasi kikubwa haijitokezi waziwazi kwa msomaji au msikilizaji wa kawaida.Diskosi hii ni eneo lenye historia inayorudi  nyuma Hadi miaka 70,na ilitokana na kundi la wanaisimu pamoja na wananadharia wa kisanaa.(Fowler na wenzake,1979;Kress na Hodge,1979).Nadharia hii ilikitwa kwenye mtazamo wa sarufi amilifu iliyoasisiwa na Halliday.Wanadiskosi hakikifu changanuzi waliegemea maono yao kwenye mwelekeo wa Halliday,huku wakiangalia matumizi ya lugha Kama yanayotekeleza majukumu yafuatayo;
(i) Uamilifu wa kiutambuzi na jinsi ya kufikiri
(ii) Mahusiano Kati na baina ya watu.
(iii) Uamilifu wa kimatini.
Diskosi hakikifu changanuzi huangalia pia namna wasemaji au watumiaji wa Lugha hufanya uteuzi wao wa msamiati na sarufi ama kisadfa au kwa kupanga.Uteuzi huu huwa unaongozwa na itikadi maalumu,Kama anavyoeleza Bulter 1990 pia huangalia nafasi ya hadhira katika uhakiki na uchambuzi wa diskosi .Uelewa wa diskosi wa hadhira huweza kutofautiana na ule wa msemaji .Diskosi hakikifu changanuzi ni mtazamo wa kinadharia unaounganisha mawazo ya taaluma mbalimbali, Van Dijk (1998)anaeleza kuwa Diskosi Hakikifu cahnganuzi si nadharia mahususi inayojitegemea Bali ni mtazamo ambao unajumisha mawazo na mielekeo kutoka taalum nyingine nyingi kama vile anthropolojia ,saikolojia ,sosholojia na kadhalika .Miongoni mwa wataalamu ambao wamechangia Nadharia hii ni pamoja na Van Dijk( 1998)Wodak (1996) na fairclough .(1999) wataalamu hawa wanatofautiana kwa kiasi kikubwa kwa sababu kila moja ana muegemeo,msisitizo na itikadi zinazomtawala ni katika mkabala huo wa mawazo amabapo lugha na itikadi hujiri Kama mada kuu katika diskosi hakikifu changanuzi (Van Dijk,1998). Hapa diskosi hujitokeza Kama njia ya kukuzia na kuendeleza itikadi fulani.Hata hivyo nadharia ya diskosi changanuzi imechunguzwa na wanaisimu jamii ,na wanaisimu wenye muegemeo wa kianthropojia .Kwa ujumla diskosi hakikifu changanuzi inakitwa kwenye mihimili mbalimbali Kama ifuatavyo.
Mihimili ya diskosi hakikifu changanuzi
Lugha ni mfanyiko wa kijamii ambao huuwezesha ulimwengu kuwakilishwa ,Hivyo watumiaji wa lugha huiona Kama asasi yenye uwezo mkubwa katika kutekeleza majukumu mengi .kwa mantiki hii Diskosi au matumizi ya lugha kwa ujumla ni aina ya mifanyiko ya kijamii inayoendana na matumizi na udhihirikaji wa mamlaka , utawala ,ubaguzi na upinzani .uchunguzi wa lugha huhusiana na matumizi ya lugha kwa ujumla wake.
Diskosi hakikifu changanuzi hutuwezesha kufahamu kuwa lugha hutumiwa kwa njia tofauti katika miktadha na mazingira mbalimbali, Hivyo matumizi ya lugha yafaa kuelewaka ndani ya muktadha, kwa mantiki hiyo tunaweza kutambua uhusiano uliopo Kati ya matumizi ya lugha na malengo ya yanayohusiana na matumizi hayo.
Wasemaji na waandishi hutekeleza majukumu yao kwa kuegemea mifanyiko ya kimiingiliano inayokitwa kwenye maslahi au malengo mahususi yanayotawala yale ambayo yanaweza kuingizwa au kutolewa kwa Diskosi husika .kwa mfano Diskosi ya siasa huandamana hasa na wanasiasa na taaluma ya siasa katika mapana na marefu yake
Mtazamo wa Diskosi Hakikifu Changanuzi haulengi tu kutafuta au kufasili matini, aina hii ya diskosi hutekeleza jukumu la kuhakiki na kufafanua matini za sampuli mbalimbali ,kipashio Cha uchunguzi katika taaluma ya Diskosi Hakikifu Changanuzi ni matumizi ya lugha katika miktadha na mazingira halisi ya kimaingiliano .Maumbo haya ya lugha huchunguzwa kwa kurejelea namna yavyojitokeza na kutumiwa katika miktadha mahususi ya jamii mfano matangazo ya biashara na ukuzaji wa utamaduni 
Hivyo lengo la diskosi hii Ni kuangalia namna lugha hutumiwa kwa njia tofauti katika sajili mbalimbali .kila siku watumiaji wa lugha hurejelea ghala kuu la maumbo ya lugha tofauti.
(vii). Nadharia ya utaratibu wa adabu/ukarimu
Nadharia hii hujihusisha na mambo yaliyo mazuri na yasiyokuwa na maudhi kwa baadhi ya watu wengine. Hivyo Nadharia hii huendana sambamba na mambo yaliyo katika kinyume na matakwa Utaratibu huu una kanuni nyingi zinazohusu adabu ,heshima,unyenyekevu na hulenga kutowaumiza au kuwaudhi wengine. Pia hupendekeza mambo mengi muhimu, kwamfano,         
Kanuni ya sifa; mtu apunguze ukebehi wa wengine na aongeze au azidishe sifa kwao.  
Kanuni ya ukarimu; mtu ajipunguzie faida huku akijiongezea gharama.
Kanuni ya ukubaliano; mtu apunguze kutokubaliana na wengine,aongeze kukubaliana nao
Kanuni ya stars au haya; mtu ajipunguze  kujisifu na aongeze kutojisifu.
Kanuni ya hurum; mtu apunguze kutowahurumia wengine,aongeze huruma kwao.
Kwamfano, 
Debora: sote tunampenda sana Hassan na halima au sio?
Amina: kwa hakika sote tunampenda sana Hassan 
Hapa,Amina anafuata taratibu wa ukarimu (kwa kutoonyesha chuki yake kwa halima)
Na kuacha nje ule wa ushirikiano ,hasa kanuni ya idadi ambapo anatoa kanuni zisizo za idadi
Hitimisho;
 Pamoja na kuwa pragmatiki ina nadharia mbalimbali siyo tu kuwepo kwa nadharia bali zina umuhimu kama vile kufanya mazungumzo yanaendana na muktadha kwani wazungumzaji huendana na muktadha lengwa, kusaidia namna na jinsi ya kufanya mawasiliano kwa hekima, busara .hivyo nadharia za pragmatiki zinasaidia katika kuongoza mawasiliano baina ya watu au watumiaji wa lugha.

          
                                             MAREJEO.
Massamba D.P.B.(2004).Kamusi ya isimu na falsafa ya lugha ,Dar-es-saalam .TUKI
Richmond H Thomason(2012). What is semantic?Second version ,Oxford .
Tuki.(2004). Kamusi ya kiswahili sanifu Oxford  University press ,TUKI ,Dar -es-saalam 
Yule G.(1996). Pragmatics,Oxford University press ,Hong kong
Obuchi .S.M & Nabeta,S.(2016).Taaluma ya maana ya semantiki na Pragmatiki;Jomo Kenyatta foundation;Kenya
Share This :
...